Tuesday, August 4, 2015



NAMNA anavyojua kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, akiwahimiza wenzake kukaba mpaka kivuli, huku akionyesha mfano, imemfanya beki wa kimataifa wa mabingwa wapya wa Kombe la Kagame, Azam FC , Serge Pascal Wawa kubatizwa jina la Waziri wa Ulinzi.
Jina na cheo hicho si cha kwanza kusikika hapa nchini, miaka kadhaa nyuma aliwahi kupewa Hamis Yusuf beki aliyewahi kung’ara na timu kadhaa ikiwamo Yanga na African Lyon kwa jinsi staili yake ya uchezaji ilivyokuwa kikwazo kwa washambuliaji wasumbufu.
Muulize Amissi Tambwe au Donald Ngoma wa Yanga watakufafanulia vizuri namna beki huyo wa kati ya Azam alivyokuwa akikaba mpaka vivuli vyao kiasi cha kushindwa kufurukuta na kuishuhudia timu yao ikiaga mashindano ya Kombe la Kagame yaliyomaliza juzi Jumapili.
Wawa anafahamu kitu gani kilichomleta Tanzania, thamani yake kwa Azam imelipa kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya tangu atue akitokea El Marreikh ya Sudan kuanzia kwenye Ligi Kuu mpaka kwenye Kombe la Kagame.
Ndiyo maana haikuwa ajabu katika michezo sita ambayo mchezaji huyo aliiwakilisha Azam kwenye michuano ya Kagame kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mechi mara tatu kabla ya kuibuka kuwa Mchezaji Bora wa michuano hiyo.
Mwanaspoti ilifanya naye mahojiano maalumu na kueleza mambo kadhaa ikiwamo kwa nini anaitwa Waziri wa Ulinzi wa Azam?
Ubora
Wawa anakiri kupachikwa jina hilo na wachezaji wenzake pengine kutokana na ubora wake wa kucheza kwa bidii, kujituma na kuisaidia timu na kuhakikisha hakuna straika anayeleta tabu kwa makipa wao.
Anasema licha ya changamoto kubwa anazokutana nazo kama mchezaji, bado anajitahidi kuhakikisha Azam inakuwa ikifanya vema katika kila mchezo akishirikiana na wenzake kwa kutambua kuwa bila ushirikiano ni vigumu yeye kung’ara pekee yake.

0 comments:

Post a Comment

Designed by Adamu Mwanakatwe