
YALIANZA maneno, lakini sasa Jose Mourinho na Arsene Wenger wanaelekea kubaya zaidi. Juzi kila kitu kilikuwa wazi kwamba makocha hawa wana bifu zito zaidi ya ilivyokuwa inafikiriwa awali.
Arsene Wenger hatimaye alifanikiwa kukata uteja wa
kucheza mechi 14 bila ya kushinda dhidi ya Mourinho, baada ya bao murua
la winga wake, Alex Oxlade-Chamberlain kuipa timu yake taji la Ngao ya
Jamii.
Hata hivyo, mechi hiyo iliingiwa na doa baada ya
Wenger kukwepa kumsalimia Mourinho mara mbili, huku mara ya pili ikiwa
wazi zaidi baada ya Mourinho kujipanga kuwasalimia wachezaji wote wa
Arsenal na benchi la ufundi, lakini Wenger akapita mgongoni kwake na
kuwafuata wachezaji wake.
Mourinho amesikitishwa na kitendo hicho huku
akimlaumu Wenger kwa kuukwepa mkono wake mara mbili, ingawa Wenger
amepuuza jambo hilo.
“Nilikuwa nafanya vile kwa ajili ya heshima ya
klabu yangu na heshima yangu kama meneja na inabidi nifanye vile kwa
klabu ambayo ni mshindi, unawasubiri katika namna hauwezi kukosa kumwona
mtu yeyote na hakuna atakayekosa kukuona,” alisema Mourinho.
“Kila mchezaji alikuja katika mwelekeo wangu kitu
ambacho kilikuwa rahisi kwangu kufanya, sasa kama kuna watu wengine
hawakuja katika mwelekeo wangu hilo siyo tatizo langu, siyo habari, siyo
mwisho wa dunia na sina tatizo na hilo,” aliongeza Mourinho.
“Nilifanya kazi yangu, kazi ambayo klabu yangu
inastahili niifanye kwa hadhi yangu kama bosi pindi ninapopoteza mechi
ya Ngao ya Jamii au kombe lolote lile.”
Hata hivyo, Wenger alipuuza madai hayo ya Mourinho
huku akidai kwamba alipeana mikono na watu wachache aliojisikia kupeana
nao mikono na hiyo siyo habari.
“Nilipeana mikono na watu wachache leo baada ya
mechi, lakini hakuna kitu cha maana hapo. Naamini katika kazi ambayo
inabidi uwaheshimu watu na umheshimu kila mmoja,” alisema Wenger.
Wenger pia alikanusha madai ya Mourinho kwamba
Wenger aliachana na falsafa yake ya kucheza soka la kushambulia na
kuamua kucheza soka la kujihami kwa ajili ya kulinda bao la Chamberlain.
“Hakuna tulichoachana nacho. Tulijilinda kwa
sababu kulikuwa na kikwazo cha kisaikolojia dhidi ya Chelsea kwa
wachezaji wangu. Walitaka kulinda ushindi wetu wa 1-0 kuliko kucheza,”
alisema Wenger.
“Inabidi tukubali hilo. Sidhani kama hilo ni
kuachana na falsafa yetu, ni kweli kwamba ni mechi ambayo tulitaka
kushinda na ndiyo maana tulifanya hivyo. Najivunia hilo,” aliongeza
kocha huyo Mfaransa.
0 comments:
Post a Comment