
MIEZI kadhaa iliyopita wakati ikishiriki Ligi Kuu Bara, Azam iliyokuwa mabingwa watetezi ilikuwa ikionekana kuwa ‘kimeo’. Soka lake lilikuwa halivutii na wachezaji walikuwa wakicheza bila malengo.
Ndiyo maana haikuwa ajabu kuishuhudia timu hiyo
ikipoteza taji lake kwa Yanga, baada ya kuanza msimu kichovu na kuja
kuzinduka mwishoni baada ya kupelekwapelekwa na Simba ambao walionekana
kuipania kuitwaa nafasi ya pili.
Hata hivyo kwa sasa Azam inaonekana kuwa ya
tofauti siku chache tu baada ya kukabidhiwa mikononi mwa Kocha Stewart
Hall kutoka Uingereza.
Kocha huyo anaifundisha Azam kwa mara ya tatu sasa
baada ya kuwahi kufanya hivyo miaka ya nyuma. Kipindi chote ambacho
Hall amekuwa na Azam imeonekana kuwa ya tofauti na kucheza kandanda safi
na la kuvutia.
Kocha huyo aliiwezesha Azam kutwaa mataji mawili
ya Kombe la Mapinduzi na kufika katika hatua ya mtoano ya Kombe la
Shirikisho Afrika mwaka 2012. Wakati anaondoka Azam msimu wa 2013/14
aliiacha timu hiyo ikishika nafasi ya pili kwenye Ligi ambapo pia
ilikuwa imecheza michezo 13 bila kupoteza.
Stewart mara baada ya kukabidhiwa timu amefanya
mabadiliko kidogo katika benchi lake la ufundi ambapo aliwaomba mabosi
wa timu hiyo kuleta watumishi kadhaa kutoka Uingereza.
Ukiachana na mabadiliko ya nje ya uwanja, ndani ya
uwanja Stewart amefanikiwa kufanya mabadiliko kadha wa kadha ndani ya
muda mfupi tu na huenda akafanya mengine makubwa kwa siku zijazo.
Mfumo
Msimu uliopita Azam ikiwa na makocha Joseph Omog
na baadaye George ‘Best’ Nsimbe ilikuwa ikitumia mfumo wa 4-2-3-1 na
4-4-2, lakini mara baada ya Stewart kupewa timu hiyo ameanza na mfumo wa
3-5-2 ambao unaonekana kuzaa matunda. Timu hiyo ikitumia mfumo huo
imeshinda mechi zake zote tatu za hatua ya makundi katika michuano ya
Kombe la Kagame inayoendelea ikiwa pia haijafungwa bao hata moja.
Katika mfumo wake, Mzungu huyo anawatumia mabeki
watatu nyuma ambao ni Aggrey Morris, Sergie Wawa na Erasto Nyoni na
kuwatumia wachezaji watano katikati.
Mfumo huo umeiwezesha Azam kuwa imara katika eneo
la kati ambapo hucheza viungo watatu na pia katika mashambulizi ya
kupitia pembeni ambapo mabeki wa pembeni Shomary Kapombe na Gadiel
Michael wamekuwa wakipiga mipira ya krosi ya kutosha.
Hata hivyo mfumo huu una changamoto zake na
utapata kipimo kizuri pale timu hiyo itakapokutana na timu zinazotumia
mashambulizi ya pembeni zaidi.
0 comments:
Post a Comment