
RONALDO? Hapana aisee. Ndivyo ambavyo Kocha wa Manchester United, Louis van Gaal alivyowakata maini mashabiki wa United ambao bado wanasubiri kwa hamu kuona kama Mreno huyo anaweza kurudi Old Trafford.
Van Gaal amekiri kwamba bado anatafuta
mshambuliaji staa kuongoza safu ya ushambuliaji Old Trafford, lakini
staa huyo hatakuwa Cristiano Ronaldo tofauti na baadhi ya fikra za
mashabiki ambao waliamini kuwa Van Gaal angeweza kufanya uhamisho wa
kushtukiza kumrudisha Ronaldo.
“Barcelona ina Messi, Neymar na Suarez. Tunahitaji
mchezaji wa aina hiyo,” alisema Van Gaal, ambaye inadaiwa kuwa
anakaribia kumchukua mshambuliaji wa Barcelona, Pedro kwa dau la Pauni
22 milioni.
Kuhusu dili la Ronaldo, Van Gaal alijibu “Hilo
haliwezekani kwa sababu kuna klabu, Ronaldo, pia kuna Manchester United
na kiasi gani ambacho Manchester United inataka kutumia,” alijibu
kifalsafa kocha huyo raia wa Uholanzi.
Mashabiki wa Man United wamekuwa wakiendelea
kumuota Ronaldo ambaye aliichezea klabu hiyo kwa miaka sita chini ya
utawala wa Sir Alex Ferguson baada ya kununuliwa kwa Pauni 12 milioni
kutoka Sporting Lisbon mwaka 2003.
Hata hivyo, Agosti 2009 aliuzwa kwa dau la Pauni
80 milioni kwenda Real Madrid, ikiwa ni dau la rekodi ya uhamisho wa
dunia wakati huo, kabla ya Gareth Bale hajanunuliwa kwa Pauni 85 milioni
kwenda Santiago Bernabeu miaka miwili iliyopita.
Wakati Van Gaal akiachana na mpango wa kumchukua
Ronaldo, winga wake, Angel Di Maria amepaa mpaka katika Jiji la New
Jersey kwa ajili ya kupimwa afya na kukamilisha uhamisho wa Pauni 45.9
milioni kwenda PSG ambayo ipo ziarani nchini humo.
Staa huyo ameamua kujiunga na PSG baada ya
kuchemsha katika msimu wake wa kwanza Manchester United ambayo ilimnunua
kwa dau la Pauni 59 milioni Agosti mwaka jana kutoka Real Madrid.
Hata hivyo, staa huyo wa kimataifa wa Argentina
hatacheza katika pambano la kirafiki kati ya United na PSG ambalo
linatazamiwa kufanyika wikiendi ijayo.
Kocha Louis van Gaal amekiri kwamba staa huyo anakaribia kuhama Old Trafford.
Pamoja na kuondoka kwa Di Maria, Van Gaal amefanya
uhamisho wa nguvu kwa kuwanunua mastaa sita klabuni hapo huku juzi
akikamilisha kumchukua kipa namba moja wa Argentina, Sergio Romero
ambaye alikuwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na Sampdoria
ya Italia.
Wachezaji wengine walionunuliwa na Van Gaal ni
Bastian Schweinsteiger (Bayern Munich), Memphis Depay (PSV), Morgan
Schneiderlin (Southampton) na Matteo Darmian (Torino).
0 comments:
Post a Comment