
MABAO manne aliyofunga kwenye hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Kagame anayoshiriki kwa mara ya kwanza yamemweka straika Michael Olunga matawi ya juu.
Olunga anayeichezea Gor Mahia ya Kenya ndiye
mchezaji aliyepo kwenye vinywa vya mashabiki wengi wa soka wanaofuatilia
michuano hiyo ya Kagame. Achana na kuhusishwa kwake na klabu za Simba
na Yanga zinazodaiwa kumpigia jaramba ili kumnyakua, lakini umahiri wake
uwanjani na hasa katika kufumania nyavu kumemfanya awasisimue wengi.
Mkenya huyo amejaliwa nguvu, mbio, chenga na akili ya kucheza soka mbali
na pua za kunusa mahali nyavu zilipo.
Mwanaspoti lilibahatika kufanya mahojiano na
Olunga na kuweka mambo mengi hadharani na kiu yake ya kuona anafika
mbali katika kucheza soka na hamu ya kutwaa Kiatu cha Dhahabu cha
michuano ya Kombe la Kagame inayoingia hatua na robo fainali kuanzia leo
Jumanne.
Kombe la Kagame
Hii ni mara yake ya kwanza kushiriki michuano
hiyo, lakini hata anafurahishwa na kasi aliyoingia nayo kiasi cha
kumfanya awe gumzo kubwa kwa mashabiki wa Bongo.
“Tumekuja hapa tukiwa na lengo moja, hili lipo kwa
wachezaji wote wa timu yangu, kwamba tujitume timu ipate mafanikio
makubwa, tunajua kwamba kila timu iliyokuja hapa ni bora.
“Ninashukuru tunakwenda vizuri na kwa upande wangu
nina kiwango ambacho hata mwenyewe kinanifurahisha. Lakini sijaridhika,
nimepanga kuongeza bidii zaidi kwani nataka kupata mafanikio makubwa,
hii ni vita lazima tupambane,” anasema Olunga.
Kujiuza
Michuano ya Kombe la Kagame imekuwa ikitumiwa na
wachezaji wengi kujiweka sokoni na klabu kuingia kwenye vita ya kusaka
wachezaji, hasa kwa klabu za Ligi Kuu ya Tanzania Bara kama Yanga, Simba
na Azam.
Klabu hizo zimekuwa zikitajwa kumwinda Olunga na
kuahidi kumng’oa katika klabu yake ya Gor Mahia anayoichezea kwa msimu
wa kwanza.
Hata hivyo, Olunga mwenyewe anasema klabu hizo
zinazomsaka ni kama zinajisumbua tu, kwa sababu hana mpango wa kuachana
na Gor Mahia maarufu kwa jina la Kagalo kwa hivi sasa.
“Sijapata ofa yoyote kutoka timu hizo, hakuna
aliyenifuata, hata hivyo, siwezi kulizungumza zaidi suala hilo kwani
nina mipango yangu, kwanza nataka kuisadia timu yangu itwae taji la
Kagame na Ligi Kuu Kenya (KPL),” alisema.
0 comments:
Post a Comment