Wednesday, July 29, 2015




KIUNGO Mwinyi Kazimoto amekubali kurudi Simba kwa dola 25,000 sawa na Sh50 milioni ambapo dau hilo ni zaidi ya mshahara wa mwezi wa Rais wa Guinea, Alpha Conde, ambaye analipwa dola 22,000 kwa mwezi.
Kwa mujibu wa uchambuzi wa mtandao wa African Review, Rais huyo ni miongoni mwa marais kumi wa Afrika wanaolipwa mishahara midogo.
Kwa Afrika Mashariki Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ndiye anayelipwa kidogo zaidi ambapo mshahara wake kwa mwezi ni dola 13,000(Sh26 mil), Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta analipwa dola 132,000(Sh268 mil).
Uchunguzi wa mtandao huo umedai kwamba Rais wa Rwanda, Paul Kagame dola 85,000 (Sh173 mil) na Rais Jakaya Kikwette analipwa dola 192,000 (Sh390 milioni), Kikwette ndiye Rais anayelipwa zaidi Afrika Mashariki.
Turudi kwa Kazimoto. Mshahara wa Kazimoto kwa mwezi ni analipwa Sh2 milioni ambapo amesaini mkataba wa miaka miwili. Kwa maana hiyo, Kazimoto ataikomba Simba jumla ya Sh 98 milioni kwa miaka miwili ambapo fedha ya usajili ni Sh 50 milioni wakati mshahara kwa miaka miwili ni Sh 48 milioni.
Habari kutoka ndani ya Simba, zinasema kuwa kiungo huyo ambaye pia alikuwa akiwaniwa na Azam FC atajiunga na wenzake keshokutwa Alhamisi katika kambi yao iliyopo visiwani Zanzibar ikiwa ni pamoja na straika wao mpya, Laudit Mavugo aliyedaiwa kuwa ataingia leo Jumanne au kesho Jumatano akitokea kwao Burundi.
Dili la kumsajili kiungo huyo, lilianza kufanywa kimya kimya ambapo wiki iliyopita Ijumaa viongozi wa Simba walimkalisha chini na kuzungumza naye ambapo wao walitaka kumpa dolla 20,000 ambazo Kazimoto alizikataa na kutaka apewe dola 25,000 ambazo Simba wamempa.
Kazimoto yupo nchini kwa muda sasa baada ya timu yake ya Al Markhiya ya Qatar kuachana naye kutokana na mabadiliko ya sheria za usajili nchini humo ambazo zinazitaka kila klabu kuwa na wachezaji watatu wa kigeni.
“Mwinyi amekubali kusaini baada ya viongozi kukubali kumpa fedha hiyo ingawa wenyewe walikuwa wanataka ashuke zaidi,” alisema kiongozi huyo.
Usajili wa mchezaji huyo umethibitishwa na Rais wa Simba, Evans Aveva “Ni kweli amesaini mkataba na tutakuwa naye kwa kipindi hiki, hiyo imekuja baada ya kufikia makubaliano.”

0 comments:

Post a Comment

Designed by Adamu Mwanakatwe