
KIMEELEWEKA Jangwani baada ya Yanga jana Ijumaa kupata ushindi
wa mabao 2-0 dhidi ya KMKM ya Zanzabir, na kutinga robo fainali ya
michuano ya Kombe la Kagame huku ikipania ushindi zaidi kwenye mchezo
ujao kesho Jumapili dhidi ya Al Khartoum.
Mabao ya kipindi cha pili yaliyotumwa kimiani na
Malimi Busungu na jingine la kujifunga la beki wa KMKM, Ali Nassor,
yalitosha kuihakikishia Yanga moja ya nafasi tatu za kundi la A
ikiungana na Al Khartoum ya Sudan na Gor Mahia ya Kenya zilizotangulia
mapema katika hatua hiyo.
Pambano hilo lililochezwa Uwanja wa Taifa, jijini
Dar es Salaam, lilishuhudia timu hizo zikienda mapumziko bila ya bao
lolote licha ya kosakosa nyingi kwa kila timu.
Busungu aliyesajiliwa Yanga akitokea Mgambo JKT,
alifunga bao ambalo kwake ni la tatu katika michuano hiyo. Alifanya
hivyo katika dakika ya 56 kutokana na juhudi binafsi baada ya kupokea
pasi na Geofrey Mwashiuya na kumzidi maarifa beki ya KMKM kabla ya
kumtungua kipa Nassor Abdallah.
Mara baada ya Busungu kufunga bao hilo, Yanga
iliendelea kufanya kosa kosa kupitia kwa mastraika wake wapya, Donald
Ngoma aliyeisumbua sana ngome na KMKM akisaidiwa na Mwashiuya.
Hata hivyo Busungu alipumzishwa na nafasi yake
kuchukuliwa na Amissi Tambwe ambaye kukurukakara zake ziliisaidia Yanga
kuandika bao la pili katika dakika ya 73 baada ya beki wa KMKM, Ali
Nassor kujifunga katika harakati za kuokoa wakati akiwania mpira na
Tambwe.
Kwa ushindi huo wa jana Yanga imefanikiwa
kung’ang’ania nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi lao kwa kufikisha
pointi 6 ikisaliwa na mechi moja dhidi ya vinara wa kundi hilo Al
Khartoum ambayo mapema mchana ililazimishana sare ya bao 1-1 dhidi ya
Gor Mahia.
Timu hizo mbili ambazo kama Yanga zimesaliwa na
mechi moja moja kila moja ina pointi 7 na zitamaliza mechi zao siku ya
Jumanne kwa Yanga kuumana na Al Khartoum na Gor Mahia kupepetana na
Telecom ambayo ilishaaga mashindano hayo. KMKM imeshamaliza mechi zake
ikiwa na pointi 3 ikimaliza katika nafasi ya nne.
Kwa ujumla pambano la jana lilikuwa kali na KMKM
ilionyesha ilivyolipania pambano hilo kama ilivyokuwa katika mechi zao
za awali, lakini katika kipindi cha pili baada ya kutunguliwa bao moja
walilegea na kuipa nafasi Yanga kutawala, ingawa Jangwani itajilaumu kwa
kushindwa kuibuka na ushindi mnono kutokana na washambuliaji wake
kukosa umakini langoni mwa KMKM.
Baada ya mchezo Ngoma alitangazwa Mchezaji Bora wa Mechi.
Katika pambano la mapema mchana, Gor Mahia
iling’ang’aniwa na Al Khartoum baada ya kutoka sare ya 1-1. Timu hizo
zimetinga robo fainali zikiungana na APR ya Rwanda na Al Shandy za Kundi
B na Azam ya Kundi C.
KMKM: Nassor Abdallah, Pandu
Haji, Said Idrissa, Khamis Ali, Mussa Said, Ibrahim Khamis, Juma Mbwana,
Tizo Chombo, Nassor Ali/Fakhi Sharif, Haji Simba na Mateo Simon
0 comments:
Post a Comment