Thursday, June 26, 2014

HATARI: Kombe la Dunia 2014 litaondoka na mastaa hawa


Umri wa sasa wa mchezaji huyo ni miaka 36, hadi kufikia fainali zijazo za Kombe la Dunia nchini Urusi, Drogba atakuwa na umri wa miaka 40 kitu ambacho kitakuwa kigumu kwake kucheza fainali hizo. 

RIO DE JANEIRO, BRAZIL
KIUNGO Mhispaniola, Xabi Alonso, ameripotiwa kutangaza kustaafu soka la kimataifa baada ya nchi yake ya Hispania kutolewa kwenye hatua ya makundi katika fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea kule Brazil.
Staa huyo wa Real Madrid amekuwa kwenye kikosi cha kwanza cha Hispania tangu mwaka 2003 na kufanikiwa kufunga mabao 16 katika mechi 113 alizochezea nchi hiyo na pia kuwamo kwenye vikosi vilivyotwaa ubingwa wa Ulaya mara mbili mwaka 2008 na 2012 na Kombe la Dunia mwaka 2010.
Hata hivyo, Alonso ni mmoja tu wa mastaa kadhaa ambao baada ya fainali hizi za Kombe la Dunia hawataonekana tena kwenye nchi zao wakati wa fainali zijazo za mwaka 2018 zitakazofanyika Urusi.
Andrea Pirlo, Italia
Kiungo huyo fundi raia wa Italia alitangaza mapema kwamba atang’atuka kwenye soka la kimataifa baada ya kumalizika kwa fainali hizi za Kombe la Dunia.
Hata hivyo, kulingana na umri wake wa miaka 35, Pirlo asingeweza kuwa na nguvu tena ya kucheza fainali zijazo zitakazofanyika miaka minne baadaye hasa kutokana na soka la kisasa ambalo limekuwa likichezwa kwa kasi.
Pirlo ambaye pia ni kiungo wa Juventus, amekuwa kwenye kikosi cha Italia tangu mwaka 2002 na kuwamo kwenye kikosi hicho kilichonyakua ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka 2006. Kwa kipindi chote alichokuwa na Italia, Pirlo amecheza mechi 111 na kufunga mabao 13.
Didier Drogba, Ivory Coast
Straika Didier Drogba amekwenda kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil akiwa mmoja wa wachezaji wenye umri mkubwa katika kikosi cha Ivory Coast.
Umri wa sasa wa mchezaji huyo ni miaka 36, hadi kufikia fainali zijazo za Kombe la Dunia nchini Urusi, Drogba atakuwa na umri wa miaka 40 kitu ambacho kitakuwa kigumu kwake kucheza fainali hizo.
Kwa hali ilivyo, fainali hizi zinatajwa kuwa za mwisho kwa Drogba na kizazi kingine cha dhahabu cha Ivory Coast ambacho kimeshindwa kufanya maajabu kwenye michuano ya kimataifa.

0 comments:

Post a Comment

Designed by Adamu Mwanakatwe