KUTOKA LONDON: England ni kulaumiana tu

PAMOJA na kwamba Waingereza hawakutarajia timu yao ya taifa
kutwaa Kombe la Dunia, lakini wamefadhaishwa na matokeo ya England
katika mechi zake mbili za mwanzo.
Tangu Alhamisi hadi sasa mitaani jijini hapa,
kwenye redio utitiri za FM za Uingereza gumzo ni timu ya Taifa ya
England. Lawama nyingi zinaelekezwa kwa mabeki na kiungo licha ya kwamba
hata ushambuliaji haujajijenga vyema.
Lawama pia zinatupwa kwa kocha, Roy Hodgson, kwa
jinsi alivyokuwa akijitapa na kuwapa moyo washabiki kwamba wanakwenda
kushindana hasa.
Baada ya kufungwa na Italia kwenye mechi ya kwanza, wakabamizwa tena na Uruguay 2-1, muuaji wao akiwa Luis Suarez.
Nakumbuka Alhamisi ile baada ya jina la Suarez,
mpachika mabao wa Liverpool kutajwa kwenye orodha ya Uruguay, jamaa
wengi niliokuwa nao waliguna kwa uchungu uliochanganyika na hasira.
Walihisi kwamba angewadhuru; hawakutarajia
angecheza maana kwenye mechi ya Italia hakucheza na ni mwezi mmoja tu
uliopita alikuwa akiburuzwa kwenye kiti cha magurudumu baada ya kuumia
kwenye mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Newcastle.
Waingereza hapa wameudhika zaidi kwa sababu Suarez
anacheza timu moja na nahodha wa timu ya taifa, Steven Gerrard na
mshambuliaji mahiri, Daniel Sturridge.
Suarez ambaye mwaka 2010 aliizuia Ghana isifike
robo fainali kwa kudaka mpira uliokuwa unatumbukia wavuni, anacheza pia
na akina Raheem Sterling na beki Glen Johnson ambaye analaumiwa pia kwa
kuwa uchochoro.
Maudhi ya Waingereza ni kwamba Suarez huyu huyu
amewahi kudai kwamba Chama cha Soka England (FA) na vyombo vya habari
vya hapa havimpendi wala havimtendei haki na angetaka kwenda kucheza
ligi ya nje ya hapa.
Lakini wangekuwa na kikosi imara hawangekuwa na
sababu ya kusikitika kuona mchezaji fulani wa upinzani yupo wala sababu
ya kuwapangia makocha wapinzani kikosi.
Nimesikia mashabiki wengi wakiwa na mawazo kwamba palikuwa na haja ya wachezaji wakongwe kujumuishwa kikosini.
Wanaona ilikuwa makosa kumwacha Ashley Cole hata
kama ameshuka kiwango na pia wangemwita John Terry, nahodha wa zamani
ambaye alisema angekuwa tayari kurudi kikosini kama angeitwa licha ya
kutangaza kustaafu.
0 comments:
Post a Comment