
Wachezaji wa timu ya Yanga wakishangilia wakati wa msimu wa ligi kuu uliopita
DAKTARI wa Yanga, Juma Sufiani amewaasa wachezaji wa timu hiyo
kujiepusha na vitendo vya ulevi katika kipindi hiki cha mapumziko na
atakayekiuka ataona matokeo yake uwanjani msimu ujao.
“Wachezaji wanatakiwa kujiweka mbali na matumizi
ya vitu kama pombe kwa kipindi hiki, wasijiachie sana kwasababu ni
mapumziko bali wazingatie kupata mlo mzuri na kufanya mazoezi mepesi
kwani hivyo ndivyo vitakavyowajenga.
“Ni jukumu la mchezaji mwenyewe kuielewa kazi yake
na kufuata yale tunayowaasa, kazi yetu kama madaktari ni kuwaelimisha
wao kufuata mambo yatakayowajenga, hatuwezi kuwafuatilia hata kwa
kipindi walichokuwa kambini tuliacha jukumu hilo kuwa lao,” alisema
Sufiani
Kwa upande mwingine Daktari wa Simba, Yassin Gembe
amewataka wachezaji kuhakikisha wanapata mazoezi yasiyopungua muda wa
wiki sita kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi ili kujiepusha na
hatari ya kupata majeraha yasiyo ya lazima.
“Kitaalam mazoezi ya wiki zisizopungua sita ni ya
lazima kwa mchezaji kabla ya kuanza kwa msimu mpya, wengi wanachelewa
kambini na kushindwa kufanya mazoezi kwa kipindi cha muda huu unaotakiwa
hivyo kujiweka hatarini kupata majeraha wakati ligi itakapoanza kutimua
vumbi,” alisema Gembe.
0 comments:
Post a Comment