
Jaji Mstaafu Damian Lubuva
Dar es Salaam. Serikali imeeleza nia yake ya
kufanya maboresho kwenye Daftari la Wapigakura katika mwaka huu wa fedha
2014/15, ikitumia mfumo wa biometric ambao, hata hivyo, unalalamikiwa na vyama vya upinzani nchini.
Uamuzi huo wa Serikali unafanyika ikiwa imepita
miaka mitano tangu daftari hilo liboreshwe kwa mara ya mwisho Machi
2009. Hii ni kabla ya kufanyika kwa uchanguzi mkuu mwaka 2010 wakati
kambi ya upinzani bungeni ilipoeleza wazi kutilia shaka mfumo huo.
Kwa upande wake, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imepanga kuboresha daftari hilo kwa awamu mbili kwa mfumo huo wa bionetric ili kuondoa kasoro zilizojitokeza katika mfumo wa awali wa Optical Mark Recognition(OMR).
Msimamo wa NEC
Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva
anasema lengo la tume hiyo ni kuhakikisha uboreshaji wa daftari huo kwa
awamu ya kwanza unakamilika, ili kuwawezesha watu wengi zaidi kushiriki
katika mchakato wa kura ya maoni.
Anasema Jaji Lubuva kuwa mfumo wa biometric
ambao wanatarajia kuutumia una uwezo wa kumtambua mpigakura kwa alama
za mwili, ikiwamo alama za vidole au mboni ya jicho, lengo likiwa ni
kuhakikisha uandikishaji unafanyika kwa kiwango ambacho kitaondoa
malalamiko au maswali kutoka kwa wadau.
Jaji Lubuva anasema awamu ya kwanza itafanyika
Septemba hadi Desemba, kwa kuandikisha watu wote upya, pamoja na
watakaotimiza umri wa kupiga kura yaani miaka 18 katika Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba mwakani.
Awamu ya pili inatarajiwa kufanyika kati ya Aprili
hadi Agosti mwakani na wapigakura waliohama kutoka sehemu moja kwenda
nyingine nchini watapata fursa ya kurekebisha taarifa zao.
Awamu hii ya maboresho pia inatarajiwa kuwaondoa
wapigakura waliofariki au kupoteza sifa na wapigakura wakiwamo
watakaokuwa wamepoteza kadi au kadi zao kuharibika.
Tayari, imethibitika kwamba Serikali imetoa Sh39
bilioni mpaka sasa kwa maandalizi mbalimbali ya uboreshaji kwa awamu ya
kwanza, pamoja na kununua vifaa vya kuandikishia.
Jaji Lubuva anasema NEC inatarajia kuanza vikao na
wadau mbalimbali ambavyo vitajulisha jinsi mchakato huo wa uboreshaji
awamu ya kwanza utakavyoendeshwa na teknolojia itakayotumika.
Anasema wako katika hatua za mwisho za ununuzi wa
vifaa mbalimbali vitakavyotumika katika uboreshaji huo ili kuhakikisha
mchakato huo utakapoanza unakuwa katika hali ya ufanisi zaidi.
0 comments:
Post a Comment