
Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Mohamed Kessy (kushoto) akiwakwepa wabunge wa CUF, Kombo Khamis Kombo (kulia) na Ibrahim Mohammed Sanya (wa pili kushoto) walipokuwa wakimfokea nje ya Ukumbi wa Bunge mjini Dodoma jana na Mbunge wa Mikumi, Abdulsalaam Amer akijalibu kuwazuia.
Dodoma.Kelele, kukunjana na kunyoosheana vidole
jana mchana vilitawala nje ya ukumbi wa Bunge wakati wabunge wa CUF
kutoka Zanzibar walipotaka ‘kumkanya’ Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM),
Ally Keissy.
Sakata hilo la aina yake lililodumu kwa takriban
dakika 15 lilitokea saa 7:05 mchana baada ya Naibu Spika, Job Ndugai
kuahirisha kikao cha Bunge.
Wabunge hao Mussa Haji Kombo (Chakechake), Kombo
Khamis Kombo (Magogoni) na Muhammad Ibrahim Sanya (Mji Mkongwe),
walitaka ‘kumkanya’ Keissy kutokana na kile alichosema alipokuwa
akichangia Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
mwaka 2014/15 na kusema Zanzibar haichangii katika Muungano, hivyo haina
haki ya kuhoji mambo ya upande wa pili.
Kauli hiyo licha ya kulalamikiwa na wabunge wote
wa CUF kutoka Zanzibar kiasi cha kufikia hatua ya kusimama na kuomba
mwongozo wa Spika, Keissy alizidi kuwashambulia na kusema kuwa majimbo
ya Zanzibar watu wake wanaweza kukusanywa sehemu moja kwa kupigiwa
filimbi tu.
“Nyie Zanzibar idadi yenu ya watu ni asilimia 2.8
ya watu wote wa Tanzania. Sasa mnataka kupata kila kitu sawa ili iweje!
Mnataka ajira asilimia 21 na Watanganyika wakafanye kazi wapi?” alisema
Keissy.
Baada ya kuahirishwa kwa kikao hicho na wabunge
kuanza kutoka nje, wabunge hao wa CUF walikwenda kumsubiri Keissy karibu
na jengo la kantini.
Mbunge wa kwanza kumvaa Keissy alikuwa Khamis
Kombo ambaye kabla ya kumfikia alizuiwa na Mbunge wa Mpanda Kaskazini
(CCM), Moshi Selemani Kakoso.
Wakati Keissy akishangaa alitokea Haji Kombo ambaye naye alizuiwa na Mbunge wa Mikumi (CCM), Abdulsalaam Selemani Amer.
“Mimi sitaki kupigana bwana ninachokijua ni kwamba
nilikuwa nikichangia mjadala wa bajeti na nilichokisema ni ukweli
mtupu,” alisema Keissy huku akiwa amenyanyua mikono yake juu na kuondoka
eneo hilo.
“Wewe (Keissy) sijui una nini wewe. Unapenda
kutufuata fuata sana watu wa Zanzibar. Hivi una nini wewe? Hivi hujui
kuwa Tanzania ni Muungano wa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar?”
alisikika akisema Khamis Kombo.
Kwa upande wake, Sanya hata baada ya wenzake
kutawanyika eneo hilo, aliendelea kumlaumu Keissy na kuwataka wabunge wa
CCM kumuonya.
“Anapenda sana kutoa kauli mbaya dhidi ya
Zanzibar. Jamani mkanyeni mwenzenu haiwezekani kila siku awe yeye tu
anayetukashifu bungeni,” alisema Sanya huku akitulizwa na mbunge wa
Kibiti (CCM), Abdul Jabiri Marombwa.
0 comments:
Post a Comment