
VITA inaweza kuzuka Old Trafford kama kocha
mtarajiwa wa Manchester United, Louis van Gaal, atafanya kile ambacho
kinatabiriwa na wengi klabuni hapo. Kumpa kitambaa cha unahodha Mdachi
mwenzake, Robin Van Persie.
Juzi Jumapili, Van Gaal alionyesha kila dalili
kwamba Van Persie atakuwa nahodha wake mpya Old Trafford baada ya
Nemanja Vidic kutangaza rasmi kuondoka klabuni hapo kwenda Inter Milan
msimu ujao.
Van Gaal alimsifu vilivyo Van Persie kwa kudai
kwamba ni nahodha wake ambaye wanaendana katika falsafa. Kama atamchagua
Van Persie huenda kukatokea mzozo mkubwa kutoka kwa Wayne Rooney ambaye
anaamini anastahili kuvaa kitambaa hicho baada ya kuwa klabuni hapo kwa
muda mrefu kuliko Van Persie ambaye amehamia hivi karibuni.
“Van Persie ni nahodha wangu, ni mfungaji wangu
bora kwa mwaka mmoja na nusu ambao amecheza chini yangu,” alisema van
Gaal mara baada ya pambano la kirafiki dhidi ya Ecuador ambapo Van
Persie alisawazisha katika sare ya 1-1.
“Amekuwa mfungaji bora wa muda wote wa timu ya
Uholanzi, anacheza soka la uhakika na hata baada ya kurudi kutoka katika
kuwa majeruhi, amefunga bao murua. Nimefurahishwa na kiwango chake,
lakini pia ni bonge la nahodha.
“Nadhani unamfanya mchezaji awe nahodha wako
wakati mnapoendana katika falsafa na morali. Si tu suala la soka na
mbinu na kinachotokea uwanjani, bali katika maisha vile vile. Nadhani
hilo ni muhimu na naamini kuwa Van Persie na Van Gaal wako katika
falsafa moja.”
Van Persie amekuwa nahodha wa Uholanzi kwa kipindi
cha miezi 18 iliyopita na kwa sasa yupo katika kambi ya timu ya taifa
ya Uholanzi akijiandaa kukiongoza kikosi hicho katika safari ya Brazil
kucheza fainali za Kombe la Dunia.
0 comments:
Post a Comment