
Kocha wa Mbeya City.
MEI 22, mwaka huu Mbeya City itaanza harakati
zake za kuwania Kombe la Nile Basin linaloandaliwa na Baraza la Vyama
vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kwa kushirikiana na Serikali
ya Misri.
Jina kamili la michuano hii ni ‘Cecafa Nile Basin
Cup’ yaani Kombe la Cecafa la Bonde la Mto Nile. Bendera ya Tanzania
itapeperushwa na Mbeya City, timu ngeni kabisa katika soka la ushindani
Tanzania lakini imeonyesha ukomavu mkubwa.
Wakati Ligi Kuu Bara inaanza Septemba mwaka jana,
hakuna aliyewaza kama Mbeya City ingeweza kuwa moja kati ya timu kali na
tishio katika soka la Tanzania. Labda viongozi wa timu hiyo na benchi
la ufundi ndio waliowaza makali ya timu yao.
Timu hii imeonyesha kwamba, katika soka lolote
linawezekana inapokuwepo nia na malengo ya kutaka kufanikiwa, kinyume
cha hapo hakuna litakalotendeka na hakuna njia ya mkato.
Kutokana na uhodari wake, Mbeya City almanusura
ishike nafasi ya pili katika ligi lakini ikaishia nafasi ya tatu huku
ikipata matokeo mazuri katika mechi 26 za ligi ilizocheza.
Nidhamu ya wachezaji, kocha, viongozi hata
mashabiki ndicho kitu pekee kilichoifanya Mbeya City leo hii ipate
heshima kokote inakopita nchini. Heshima ya timu hii, imeziongezea
thamani jezi zake ambazo zimetapakaa kote nchini.
Sasa Mbeya City imepata nafasi ya kuiwakilisha
nchi ndani ya msimu mmoja tu, hizi ni hatua za haraka sana katika ukuaji
lakini lazima tukubali kuwa timu hii inapata inachostahili.
Tunaiamini Mbeya City kwamba itafanya vizuri
katika michuano hiyo ndio maana hakuna minong’ono yoyote pindi Cecafa
ilipoipa nafasi ya kuiwakilisha nchi baada ya Azam FC kutokuwa na nafasi
ya kucheza michuano hiyo.
Wote tupo nyuma ya Mbeya City katika kuhakikisha
Bendera ya Tanzania inapepea vizuri katika michuano hiyo kwani ushindi
wa timu hiyo ni wetu sote, wala siyo wa watu wa Mbeya na vitongoji
vyake.
Jukumu la kuiunga mkono timu hii ni letu sote na
kamwe hatuwezi kuiacha Mbeya City ikiwa mpweke katika michuano hiyo
ukizingatia uchanga wake katika soka la ushindani, tena ngazi ya
kimataifa.
Pia, hiki ni kipimo tosha kwa wachezaji wa Mbeya
City ambao wanacheza mechi za kwanza za michuano nje ya ardhi ya
Tanzania na watambue hiyo ni nafasi yao ya kipekee kujitangaza na kuuza
vipaji vyao kimataifa.
Misri ni miongoni mwa nchi chache za Afrika ambazo
ligi yake imepiga hatua ikiwa na ufadhili mkubwa unaowezesha wachezaji
wake kulipwa mamilioni ya fedha.
0 comments:
Post a Comment