Straika mpya Simba msosi sahani tatu na chapati 10
Saad Kipanga.
SIMBA iko kwenye harakati kubwa za kumnasa straika wa Mbeya
City, Saad Kipanga. Mchezaji huyo anaendelea na mazungumzo ya karibu
sana na bosi wa usajili wa Simba, Zakaria Hanspoppe na dili inaweza
kufanyika muda wowote kwani wameshaafikiana vitu vingi.
Yeye amewaambia wampe sh 30mil halafu wamalizane
na Mbeya City ambayo ana mkataba nao wa miezi sita. Hayo ni chamtoto
sikia sasa mambo ya huyu jamaa.
Ili ashibe ni lazima apige sahani tatu za chakula
zinazojitosheleza, wakati chai yake lazima iwe na chapati 10. Kipanga
anayeichezea timu ya Taifa ya Vijana U-20 ‘Ngorongoro Heroes’ ni mdogo
kwa umri kwani ana miaka 19, lakini mambo yake hayo ni sawasawa na
umbile lake la urefu na kubwa.
Kutokana na sifa hiyo, unaweza kusema Kipanga
ametoka ngoma droo na straika wa Simba, Betram Mwombeki ambaye pia ana
umbo kubwa na awali aliwahi kusema, ili ashibe ni lazima apige pleti
tatu za maana kama Kipanga.
Kipanga mwenye sifa ya kuwa na nguvu za miguu,
aliliambia Mwanaspoti: “Siwezi kuficha ukweli wangu, huwa nakula sahani
tatu za chakula tena ziwe zimejitosheleza ninapokula, ndiyo nakuwa fiti
na kushiba kabisa, tofauti ya hapo, tunakwenda tu.”
“Chai ya asubuhi mara nyingi watu huwa wanakula
chapati mbili, hizo kwangu zinapunguza njaa tu, 10 ndiyo mpango mzima,
nikila hizo ndiyo nakuwa vizuri,”alisisitiza Kipanga.
0 comments:
Post a Comment