Saad Kipanga.
MSHAMBULIAJI wa Mbeya City, Saad Kipanga, amekiri kuwa Simba
imemfuata na yeye amewapa masharti yake, kwanza wamkabidhi kitita cha
Sh30 milioni akiweke kibindoni na mambo mengine wamalizane na uongozi wa
klabu yake.
Kipanga ni yule mshambuliaji aliyekuwa anavalia
jezi namba 27 mgongoni, mrefu na amejazia, wengi walikuwa wanamfahamu
kutokana na staili yake ya kucheza soka ya kuvizia, huwa haeleweki ni
nafasi gani ya ushambuliaji anayocheza uwanjani, kila kona anakuwepo.
Anasifa nyingine ya nguvu za miguu, mabao yake mengi ameyafunga nje ya 18 pamoja na akili ya mpira.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kipanga alisema: “Mimi
ni mchezaji wa Mbeya City na bado nina mkataba nao, ni kweli Simba
wamenifuata na tuko kwenye mazungumzo ambayo kama mambo yataenda vizuri,
nitamalizana nao.
“Lakini nimewapa masharti ambayo kwa upande wangu
nahitaji shilingi milioni 30 na mambo mengine yanayobakia, wamalizane na
klabu yangu ya Mbeya City kwa sababu bado nina mkataba nao.”
Kipanga alisajiliwa na Mbeya City usajili wa
dirisha dogo na kucheza mzunguko wa pili kwa mkataba wa mwaka mmoja
akitokea Rhino ya Tabora. Kwa kipindi hicho kifupi, ameng’ara na Mbeya
City ambayo imemaliza ligi ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo nyuma ya
Azam FC ambao ndiyo mabingwa na Yanga washindi wa pili.
0 comments:
Post a Comment