Kocha Yanga azuia manoti ya usajili wa Mbuyu Twite
Mbuyu Twite.
INAWEZA ikawa ahueni au pigo kwa Yanga, kwani Kocha wa Yanga
Hans Pluijm amesema kuanzia sasa hakuna mchezaji atakayelipwa fedha zote
za usajili wakati viongozi wakifikiria jinsi ya kumalizana na beki wake
Mbuyu Twite aliyetaka apewe chake chote.
Pluijm raia wa Uholanzi ameamua kuweka mfumo huo
kutokana na usumbufu wa wanasoka wa Afrika kutokana na uzoefu wake,
hivyo ameagiza kuanzia sasa usajili wowote utakaofanywa na klabu yake
lazima mchezaji alipwe nusu au sehemu ya fedha za usajili tu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Pluijm
alisema amekutana na mabosi wa Yanga ambao walitaka maoni yake hasa
katika kipindi hiki cha usajili na amewaambia mkakati wake huo
utakaonusuru fedha za klabu kwa wachezaji wasiowajibika ipasavyo.
Kocha huyo alifafanua kuwa katika mambo
aliyoyapinga ni wachezaji kupewa fedha zao zote za usajili wakati
wakianza mwaka wao wa kwanza wa ajira.
Pluijm alisema kwa uzoefu wake wa miaka 10 katika
kufundisha klabu za Afrika amegundua usumbufu mkubwa wa wachezaji baada
ya kupewa fedha zote za usajili mwaka wa kwanza na hivyo hataki kuona
usumbufu wa aina hiyo unatokea wakati wa utawala wake.
Kocha huyo ana uzoefu wa kufundisha soka la Afrika
kwa miaka zaidi ya 10 akiwa amewahi kufanya kazi kwa vipindi tofauti na
klabu za Ghana za Medeama SC, Berekum Chelsea, Heart of Lions Kpando na
Ashanti Gold SC.
Pluijm alisema pia amesikia taarifa za Twite
anayetaka kupewa fedha zote, kwanza akakiri kuwa bado anamuhitaji
mkongwe huyo ingawa akaagiza nyota wote watakaosajiliwa kuanzia sasa
wasipewe fedha zao zote wakati yeye akiwa kocha Yanga.
Hata hivyo kocha huyo amewataka mabosi wa Yanga
kuheshimu ahadi za kumalizana na wachezaji haraka katika mwaka wao wa
pili unapoanza ili yasiwepo malalamiko kuhusu malipo jambo alilosema
linapoteza ufanisi wa wachezaji katika timu.
“Nimewaambia viongozi kuwa sikubaliani na suala la
mchezaji kupewa fedha zote mwaka wa kwanza wa usajili, kama wakiingia
mkataba na mchezaji yeyote mfano uwe wa miaka miwili basi wampe nusu ya
fedha, zinazobaki apewe katika mwaka wake wa pili wa mkataba,”alisema
Pluijm.
“Nawajua wachezaji wa Afrika, ni wasumbufu katika
mwaka wao wa pili baada ya kumaliza fedha endapo utampatia zote, ukiacha
hilo pia nimewaambia kuhusu kuheshimu makubaliano, wahakikishe
wanamalizana na wachezaji kwa wakati si kuwapiga chenga,”alisema.
Kama uongozi wa Yanga utaheshimu agizo hilo,
huenda Emanuel Okwi akaathirika kwani alisajiliwa kwa dola 100,000 hivi
karibuni na anaidai timu hiyo salio lake la dola 40,000 ndio maana
akasusa kucheza mechi za mwisho za msimu uliopita.
0 comments:
Post a Comment