Ben alikuwa anampenda sana Joanita siku
zote alikuwa tayari kumsaidia katika kila jambo, Kijana huyu alikuwa ni
mfanyabiashara mkubwa ambaye alikuwa akijiweza katika mambo mbalimbali
yaani pesa kwake ilikuwa siyo tatizo. Joanita alikuwa ni mwanafunzi wa
chuo cha uhasibu na kwa wakati huo alikuwa akimalizia mwaka wa mwisho wa
masomo yake. Baada ya kumaliza chuo Joanita alitamani kwenda kusoma
nchini Marekani, ambapo alifikiria kumuomba mpenzi wake amsaidie kwani
wazazi wa Joanita walikuwa hawana uwezo na hata chuo miaka miwili ya
mwisho Ben ndiye aliyekuwa akimlipia ada. Baada ya kumueleza Ben nia
yake ya kutaka kwenda kusoma Marekani, mwanzoni Ben alikuwa akisita na
kumtaka aendelee kusoma hapahapa Tanzania.
Lakini Joanita aliendelea kumbembeleza
hadi Ben alikubali kwani alitakiwa kwenda kusoma kwa mwaka mmoja na
baada ya hapo arudi nchini Tanzania.Taratibu za safari zilianza na Ben
alijipanga kumuandalia kila kitu kipenzi chake Joanita, alifanya mipango
yote hadi sehemu ambayo Joanita angefikia huko Marekani alikuwa na
ndugu yake ambaye alimjulisha kuhusu safari ya Joanita. Siku zote Ben
alimsihi Joanita akasome kwa bidii, na asisahau kuwa anampenda sana
katika maisha yake na pindi tu atakapomaliza wangefunga pingu za
maisha.
Hatimaye siku ya safari ilifika na sasa
Joanita aliondoka na kumuacha Ben akiwa mpweke, Kwa upande wa wazazi wa
Joanita walimshukuru sana Ben, kwa kumjali mtoto wao. Baada ya wiki moja
Ben alikuwa akiwasiliana na Joanita kila siku huku akimtaka asome kwa
bidii, Maisha yaliendelea ikapita kama miezi saba tokea Joanita aondoke
taratibu mawasiliano yakaanza kupungua na hata namba aliyokuwa
akiwasiliana na Joanita ilikuwa haipatikani.
Ben alipata hofu nakuhisi labda Joanita
atakuwa amepatwa na matatizo kwani siku zilienda na hatimaye mwaka
uliisha ambao Joanita ndiyo alikuwa amemaliza masomo yake , lakini kwa
kipindi cha miezi mitatu kulikuwa hakuna mawasiliano kati ya Joanita na
Ben, Baadaye Ben aliamua kumpigia simu yule ndugu yake wa Marekani aende
katika chuo alichokuwa anasoma Joanita kumuangalia labda atakuwa na
matatizo, Yule ndugu yake alienda moja kwa moja hadi kule chuoni ambapo
palikuwa na umbali kama kutoka mkoa mmoja kwenda mkoa mwingine takribani
masaa kama saba, kwa usafiri wa basi.
Alipofika pale chuoni alimuulizia, na
ndipo alipokutana na baadhi ya wanafunzi ambao walikuwa wakimfahamu,
mmoja kati ya wale wanafunzi aliyejitambulisha kwa jina la Eli akasema
"Joanita si ameenda Tanzania kumtambulisha mume wake, kwani walifunga
ndoa na kaka mmoja wa kizungu, lakini baadaye Joanita alisema atampeleka
mume wake Tanzania halafu atarudi kuendelea kuishi Marekani" Kaka yule
aliyetumwa kwenda kumuulizia alibaki ameduwaa asiamini maneno aliyokuwa
anaambiwa ilibidi aulize mara mbimbili "Ati Joanita kaolewa? Na mzungu?
Halafu wameenda Tanzania? Lini? mmmh haiwezekani".
Eli alimtizama na kuchukua simu yake
kisha akaanza kumuonyesha picha mbalimbali ambazo zilimuonyesha Joanita
akiwa na mzungu katika siku yake ya ndoa. Kaka yule alimuomba yule dada
amtumie zile picha katika simu yake ya mkononi, na baada ya hapo
aliondoka huku akiwaza ni namna gani anaweza kumjulisha Ben kile
alichokutana nacho. Baadaye alifikiria na kuamua kumueleza ukweli Ben
kuwa Joanita ameolewa na mzungu Ben hakumuamini ndipo alipoamua kumtumia
picha za Joanita akiwa anafunga ndoa.
Masikini Ben alikuwa kama
amechanganyikiwa moja kwa moja aliamua kwenda nyUmbani kwa kina Joanita.
Alipofika aliwakuta wazazi wa Joanita ambao walimweleza kuwa Joanita
alikuwa ameondoka siku hiyo asubuhi Ben alikuwa akilia kama mtoto mdogo
huku akiwalaumu wazazi wa Joanita ambao walimfahamisha kuwa walikuwa
hawajui chochote kinachoendelea kwani mtoto wao amewashangaza pia kwa
uamuzi aliouchukua. Baada ya muda kidogo Baba yake Joanita alinyanyuka
na kuingia chumbani ambapo alirudi na kumletea barua aliyoiandika
Joanita kwa Ben.
"Asante sana kwa kila jambo
uliloweza kunisaidia katika maisha yangu, najua ulinipenda sana,
nashindwa namna ya kujielezea lakini naomba unisamehe Ben, Moyo wangu
umeamua kuwa na mwanaume mwingine ambaye naamini nampenda sana,
nakutakia maisha mema naamini utampata mwanamke atakayekupenda maisha
yako yote. Naomba unisamehe kwa yote yaliyotokea. Kila la heri katika
maisha yako Ni mimi Joanita."
0 comments:
Post a Comment