Niyonzima akiwa katika pozi ya picha na familia yake jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga.
Wapo waliodai amejiondoa mwenyewe kikosini
makusudi ili kuficha aibu kwa sababu kiwango chake kimeshuka, wengine
walidai ana matatizo na benchi la ufundi chini ya kocha Mholanzi, Hans
Van Pluijm.
Ndipo Mwanaspoti, ikaamua kumtilia miguu ili
kujionea na kuzungumza naye kwa undani juu ya suala hilo. Ilikuwa
nyakati za jioni nyumbani kwa mchezaji huyo ambaye anaishi Magomeni,
Makuti jijini Dar es Salaam.
Hapo anakaa pamoja na familia yake; mkewe
anayeitwa, Naillah ambaye ni Mnyarwanda mwenzake, mtoto wao wa kiume ,
Ramsey, kaka zake, Hamduni na Prezo na ndugu na jamaa wengine.
“Nimepata matatizo makubwa kwenye kipindi hiki kwa
sababu haijawahi kunitokea na kwangu naona mapya,” anasema Niyonzima
baba wa watoto wawili binti mmoja, Halila (9) na Ramsey (5).
“Watu wanazungumza tu, unajua anaweza kuibuka mtu
mwenye nia mbaya akatunga yake ilimradi kumharibia mtu. Ukweli kamili ni
kwamba, nilikuwa mgonjwa. Nimeumwa sana malaria na baadaye walikuja
kunigundua na homa ya matumbo.
“Kwa anayekumbuka nilipokuwa Misri kwenye mechi ya
marudiano na Al Ahly muda mchache kabla ya kuanza, niliondolewa
kikosini kwa sababu ya malaria, nikashindwa kucheza.
“Nilitumia dawa, tukarudi Dar es Salaam baadaye
nikapata nafuu na kuanza mazoezi na wenzangu hata ile mechi na Mgambo
JKT niliingia kipindi cha pili kumpokea Ngassa (Mrisho). Lakini baadaye,
niliumwa sana na baada ya vipimo niligundulika na homa ya matumbo
pamoja na malaria kali,”anasema Niyonzima.
“Siku hiyo nilikuwa nyumbani ndipo nikazidiwa na
kukimbizwa hospitali ambako daktari aliamua nipumzishwe kwa kulazwa
ilikuwa ngumu kujiuguza nikiwa nyumbani (anaitaja hospitali hiyo inaitwa
Nikwezi ipo Magomeni).
“Wakati huo mechi za ligi zilikuwa zinaendelea
hadi kuja kupata nafuu, zilikuwa zimesalia mechi mbili tu na hapo
nilikuwa sina nguvu na uchovu wa ugonjwa, sikuwa fiti kwa ujumla,
nikaamua nijitibie hadi nipone kabisa.
“Lakini nilichokuja kukisikia baadaye hakika
siamini kwangu naona ni makubwa, nasumbuliwa sana ndugu na jamaa
wakitaka kujua kilichonikuta. Simu nyingi zinapigwa kutoka nyumbani
Rwanda kuwa nimeondolewa Yanga ndiyo maana sichezi, wakati siyo kweli,”
anafafanua Niyonzima.
“Kusema ukweli, kitendo hicho kimenisikitisha
sana, watu hawajui utu, mimi ni mchezaji mkubwa, hata siku moja siwezi
kuogopa mechi, nimekaa Yanga na kupitia vipindi tofauti vigumu na raha.
Tulifungwa na Simba bao 5-0 mbona sikukimbia ijekuwa hizi mechi za
kawaida kwa mchezo upi?
0 comments:
Post a Comment