AZAM na Simba kwa nyakati tofauti zimeanza operesheni za
kuimarisha timu zao kwa kufanya usajili ambao huendahatima yake
ukaiachia Yanga kilio kikubwa. Azam tayari imeshamng’oa Didier Kavumbagu
na sasa inamalizana na Frank Domayo na Mbuyu Twite.
Lakini Simba imepania kuwarejesha beki Kelvin
Yondani na kipa Ally Mustapha ‘Barthez’ ambao wote ni wazoefu. Lakini
pia inamwania straika mmoja mzalendo wa Jangwani ambaye haijataka
kuliweka wazi jina lake.
Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga, aliliambia
Mwanaspoti jana Jumatano kwamba wanamtaka Barthez kwa udi na uvumba na
atatua Msimbazi kwa mkataba wa miaka miwili kama mambo yakienda kama
yalivyo sasa.
Barthez amemaliza mkataba wake na Yanga na hakuwa
na wakati mzuri kwenye kikosi hicho mwishoni mwa msimu uliomalizika
baada ya kupoteza namba yake.
Kamwaga alisema kuwa kocha wao, Zdravko Logarusic,
ndiye aliyependekeza Barthez asajiliwe ili kuongeza nguvu kwenye kikosi
chao msimu ujao baada ya kuvutiwa na kiwango chake.
“Kocha ametaka msimu ujao awe na kikosi
kisichozidi wachezaji 25 na katika mapendekezo yake pia amemtaja
Barthez. Tumeshaanza mazungumzo na Barthez na huenda tukampa mkataba wa
miaka miwili,” alisema Kamwaga ambaye ameanzisha operesheni Bunju kwa
ajili kujenga uwanja wa Simba kwenye kiwanja chao kilichoko Bunju.
Imeelezwa kuwa Barthez ameshawaweka wazi Yanga
kwamba anarudi Simba ambako alishawahi kusoteshwa benchi kwa miaka
mitatu na Juma Kaseja kabla ya kutimkia Yanga na kupanda chati na kuwa
kipa tegemeo ndani ya klabu hiyo, alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya
kufungwa mabao matatu katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba
iliyomalizika kwa sare ya mabao 3-3.
Lakini wakati Kamwaga akisema hivyo, siku moja
kabla ya kwenda kwao Croatia mapumzikoni, Logarusic aliiambia Mwanaspoti
kuwa amependekeza wachezaji sita pekee ndio wasajiliwe kwenye kikosi
chake. Alisema anataka mabeki wawili, viungo wawili na washambuliaji
wawili na kwamba alidai hataki wachezaji wa Yanga na Azam kwa vile wana
majina makubwa na ni tatizo.
“Sitaki wachezaji kutoka timu kubwa, kwanza
wanataka hela nyingi, halafu kurundika wachezaji wenye majina kunafanya
timu haifanyi vizuri, sitaki wachezaji ambao wanatembea uwanjani huku
wameshika viuno, nataka wachezaji wasio na majina kutoka timu ndogo
naamini watanisaidia, nataka mchezaji shupavu wa kikosi cha kwanza sio
mchezaji mwenye jina halafu anaanzia benchi,” alisema Loga.
Kamwaga alipoulizwa kuhusiana na kauli hiyo ya
Loga, alisema: “Loga ndiye aliyempendekeza Barthez, ripoti yake wala
haijasema kama hataki wachezaji kutoka timu hizo, yeye kapendekeza
nafasi ambazo tunatakiwa kuzifanyia kazi, hivyo suala la usajili
tumeliacha kwenye kamati ya usajili.
“Loga mwenyewe hatma yake ipo mikononi mwa uongozi
mpya utakaoingia, tayari uongozi wa sasa umeshampa hela kidogo (kishika
uchumba) ili asiende timu nyingine, lakini uongozi mpya unaweza
ukaingia na kocha wao wanayemtaka na asiwe Loga kama watafanya hivyo
uongozi wa sasa utakuwa umepoteza hela nyingi, lakini mwisho wa yote
uongozi utakaokuja ndio utaamua kila kitu,” alisisitiza.
0 comments:
Post a Comment