Friday, May 16, 2014


Kijana Amos Ng’arare Sasi (21) mkazi wa kijiji cha Kizaru wilayani Musoma Vijijni 


Kijana Amos Ng’arare Sasi (21) mkazi wa kijiji cha Kizaru wilayani Musoma Vijijni amepoteza mwelekeo wa maisha baada ya ndoto yake ya kusoma hadi chuo kikuu kuishia njiani kutokana na matatizo ya ugomjwa wa ajabu ambao umemtesa kwa kipindi cha miaka 17.
Kwa kipindi hiki kijana Amos, ambaye anatoka Kata ya Mryaza, amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu, lakini matarajio ya kupona kwa tiba za hapa nchini hayapo hivyo njia pekee iliyobaki ni kwenda nchini India kwa matibabu zaidi.
Katika mahojiano na Mwananchi wiki iliyopita akiwa Wodi Namba 21, Sewahaji, Amos alionekana mwenye mawazo kupita kiasi.
“Ndoto yangu ya elimu itakuwa imeishia hapa. Sitegemei kurudi tena. Wenzangu niliokuwa nikisoma nao darasa moja, kwa sasa wapo kidato cha nne. Nilizaliwa nikiwa sina tatizo la aina yoyote kiafya na nililelewa na wazazi wote wawili. Kwa kweli kwa malezi niliyoyapata, sikuwahi kujiona tofauti,” anasema.
“Nikiwa na miaka minne baba alifariki dunia, nikabaki na mama ambaye alitulea mimi na kaka yangu kwa furaha akijishughulisha na kilimo cha jembe la mkono,” anasema Sasi.
“Baadaye tulibaki wawili tu, yaani mimi na mama baada ya kaka kuondoka kwa madai kuwa anakwenda kutafuta maisha. Ilikuwa mwaka 1998 na mpaka leo hatujawahi kumuona wala kusikia taarifa zake,” anasimulia Sasi.
Anasimulia kuwa alipofikisha umri wa miaka minne, usoni kwake kuliota kitu kama kipele ambacho alisema kilikuwa kinamuwasha sana.
Anaongeza kuwa mama yake alimpeleka hospitali ambako alipewa dawa za kupunguza maumivu tu.
“Nilipofikisha umri wa miaka tisa hali ilizidi kwa mbaya, maumivu na uvimbe ukazidi,” anasema.
“Mama alinionea huruma akawa halali pale anapoona nalia kutokana na maumivu makali. Aliamua kunipeleka hospitali ya Musoma lakini hakukuwa na mabadiliko. Mwaka 2010 alinipeleka Hospitali ya Bugando mkoani Mwanza, huko nilifanyiwa uchunguzi, lakini ugonjwa haukujulikana.”
Anasema wakati huo matokeo ya shule ya msingi yalikuwa yametoka naye alifaulu kwenda kidato cha kwanza, lakini alishindwa kutokana na kuzidiwa na maumivu.
“Nilirudishwa nyumbani, nikawa sipati huduma ya aina yoyote. Watu walioniona walinionea huruma, wengine wakawa hawataki kuniona mitaani. Walinitishia kuwa nikionekana, nitakamatwa na wachimba madini wanichinje wachukue viungo wakafanye manbo ya kishirikina wapate madini kwa wingi,” anabainisha.

1 comment:

Designed by Adamu Mwanakatwe