Friday, May 16, 2014

Beki ataka milioni 35 asaini Simba SC

Beki wa pembeni wa Coastal Union ya Tanga, Abdi Banda.
Wilbert Molandi na Said Ally
BEKI wa pembeni wa Coastal Union ya Tanga, Abdi Banda amekubali kusaini kuichezea klabu kongwe ya Simba, lakini kwa sharti moja kubwa kuwa wampatie shilingi milioni 35.
Awali, beki huyo ambaye pia anaichezea timu ya taifa ya vijana yenye umri chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes alipendekezwa na Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans van Der Pluijm.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Banda alisema kuwa mipango na taratibu zote za usajili zimekamilika na anachosubiri ni meneja wake ambaye ni baba yake mdogo, Abdul Bosnia aliyekuwa nje ya nchi.
Banda alisema kuwa, kiasi hicho cha fedha cha milioni 35 atakachokipokea ni nje ya kuvunja mkataba wa kuichezea Coastal.
Aliongeza kuwa, mipango hiyo ya usajili huenda ikakamilika mara baada ya meneja wake huyo kurejea nchini kati ya leo Ijumaa au kesho Jumamosi.
“Ninashukuru kila kitu kimekamilika, anayechelewesha ni meneja wangu aliyepo nje ya nchi, atakaporejea nitakamilisha mambo yote.
“Nimewapa ofa yangu ninayoitaka, wamesema wapo tayari kutoa kiasi cha fedha ninachohitaji nje ya kuvunja mkataba na Coastal,” alisema Banda.
Simba imepanga kuzifanyia maboresho baadhi ya sehemu muhimu ikiwemo safu ya ulinzi kwa kusajili mabeki wa pembeni.

0 comments:

Post a Comment

Designed by Adamu Mwanakatwe