Saturday, May 17, 2014


Hussein Jumbe akiwa kazini
 
Ni huzuni. Kumbi za muziki wa dansi ziko tupu. Bendi maarufu karibu zote zilizotamba miaka ya 70 na 90 zimebaki kuwa historia. Chache zilizokuwapo tunashuhudia wanamuziki wake wakipigia viti vitupu katika baa za kawaida kabisa, zilizopo pembezoni mwa jiji la Dar es salaam.
Nini kimetokea kwa muziki huu ambao unabakia kuwa alama pekee na miongoni mwa burudani ambazo Watanzania wana kila sababu ya kujivunia, kutokana na historia kuonyesha kuwa muziki huo uliasisiwa nchini Tanzania na ulianzishwa katika Jiji la Dar es Salaam zaidi ya miaka 80 iliyopita.
Kati ya wanamuziki wakongwe nchini, Hussein Jumbe aliyewahi kupigia bendi za Msondo Ngoma na DDC Mlimani Park anapingana na wanamuziki wenzake wanaoamini kuwa muziki huo unaangushwa na vyombo vya habari.
Mfano wa kuigwa kuonyesha kuwa muziki huo bado unakubalika, ni kile alichokifanya Jumbe, akiwa na bendi yake ya Talent wiki iliyopita katika Ukumbi wa Kisumba zamani Sugar Ray uliopo maeneo ya Temeke.
Jumbe alifanya uzinduzi wa albamu ya ‘Kiapo Mara Tatu’, lakini akafanya maandalizi kama ambavyo wanafanya wanamuziki wa sasa kama vile Jahazi Modern Taarabu, Twanga Pepete, Linah Sanga, Diamond Plutnamz kwa kualika watu wengine wenye mvuto wanapokuwa wanazindua albamu zao.
Kama ilivyo kawaida yake, Jumbe licha ya kuwa ni mwanamuziki wa zamani aliachana na uzamani na kuonyesha kuwa kulialia kwamba wanamuziki wa zamani hawasaidiwi siyo dawa.
Lakini kitu kilichofanya shoo hiyo ivutie zaidi na kujiweka katika soko la muziki kama wafanyavyo wanamuziki wengine, aliweka burudani tofauti tofauti ikiwamo kikundi cha muziki wa asili cha Hayahaya Ngoma Afrika kutoka Kijiji cha Makumbusho, jijini Dar es Salaam. Kama hiyo haitoshi katika kuwavutia mashabiki wa muziki wa aina zote, hakuwatenga wadau wa taarabu kwani mwanamuziki wa miondoko hiyo Isha Mashauzi alikuwapo kuwakilisha.
Cha kufurahisha ni kwamba Isha Mashauzi, akiwa na kundi zima la Mashauzi Classic hakumuangusha kwani walifanya kile mashabiki walichokuwa wanakikusudia, ikiwamo kuimba muziki wa taarabu kwa ustadi mkubwa na kuimba nyimbo za wanamuziki wa muziki wa kizazi kipya ikiwamo wimbo ‘Maneno maneno’, wa mwanamuziki Ben Pol na kuuimba kwa ustadi mkubwa. Pia wimbo wa Injili wa mwanamuziki Bahati Bukuku‘ uitwao ‘Waraka wa Amani’ na nyimbo mbili za mwanamuziki Jumbe ambazo ni ‘nachechemea na ‘siri ya nini’.
Jumbe anena
Mwanamuziki huyo mkongwe alisema kuwa alichokifanya ni kusoma mahitaji ya soko la muziki wa sasa na kujua mahitaji ya wadau wa burudani na hatimaye hadi leo anapiga muziki na ana mashabiki vijana kwa wazee. “Niliwahi kusema kulalamika siyo dawa, tulijisahau miaka ya 80-90, tulijisahau na vijana wamechukua nafasi wanaifanyia kazi. Tunachotakiwa kufanya sasa ni kuhakikisha tunaurudisha muziki wa dansi kwenye chati ingawa kazi kubwa inatakiwa kufanyika, ”anasema Jumbe.
Jumbe anafafanua kuwa licha ya vyombo vya habari kuusahau muziki huo na wanamuziki wenyewe wanataka ujiuze kwa umaarufu wa zamani bila kujali dunia inazunguka na inakwenda sambamba na mabadiliko.“Hata Serikali imefanya mabadiliko, kulikuwa na Chama kimoja na sasa ni vyama vingi na muziki vivyo hivyo unatakiwa uende na kasi ya mabadiliko, ”anasisitiza Jumbe.
Jumbe ambaye wimbo wake wa ‘Kiapo Mara Tatu, ambao ndiyo umebeba jina la albamu hiyo, uliingia kwenye kinyang’anyiro cha tuzo za Kilimanjaro Music, katika kipengele cha Wimbo bora wa Kiswahili, ingawa haukufanikiwa kupata tuzo hiyo.

0 comments:

Post a Comment

Designed by Adamu Mwanakatwe