
Rashid Mvungi akimuangalia mtoto wake Nasrah Rashid (4) ambaye ni mlemavu wa viungo aliyefungiwa chumbani na kufichwa kwenye boksi bila ya kufanyiwa usafi tangu akiwa na umri wa miezi tisa.
Morogoro. Mwanamke aliyetambuliwa kuwa ni
Mariamu Said mkazi wa Kiwanja cha Ndege, Morogoro juzi alishushiwa
kipigo na wananchi kutokana na kumficha mtoto wa marehemu mdogo wake
kwenye boksi kwa miaka minne.
Tukio hilo lilitokea juzi saa nne asubuhi baada ya
majirani zake kutoa taarifa kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kiwanja cha
Ndege, Dia Zongo kuhusu mtoto huyo, Nasra Rashid, kufichwa ndani ya
boksi tangu akiwa na umri wa miezi tisa.
Zongo alisema majirani hao walimweleza pia kuwa jirani yao huyo hamfanyii usafi mtoto huyo wala kumtoa nje.
Baada ya kupata taarifa hizo, Zongo alimtafuta
Mwenyekiti wa Mtaa huo, Tatu Mgagala na kuongozana naye hadi kwenye
nyumba hiyo na kumhoji mwanamke huyo ambaye alikuwa akijibu kwa
kubabaika.
Moja ya maswali aliyoulizwa ni idadi ya watoto
wake na akajibu kuwa ana wawili lakini wakati akiendelea kujibu maswali,
ghafla mtoto huyo alipiga chafya na kuanza kukohoa, hivyo kuwapa
wasiwasi na kuamua kuingia chumbani kwa mwanamke huyo kwa nguvu na
kumkuta mtoto Nasra akiwa ndani ya boksi.
Ofisa mtendaji huyo alisema wakati wakimtoa mtoto
huyo ndani ya nyumba, kundi kubwa la watu waliokuwa na fimbo na mawe
walianza kumshambulia mwanamke huyo na kumlazimu mtendaji kutoa taarifa
polisi.
Alisema muda mfupi baadaye, polisi waliwasili na
kumkamata Mariam na kumpeleka katika ofisi ya kata ambako aliwekwa chini
ya ulinzi.
Baadaye aliwekwa rumande katika Kituo Kikuu cha Polisi, Morogoro na mtoto alipelekwa Ofisi za Ustawi wa Jamii.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo
alisema wanaendelea kukusanya taarifa za tukio hilo ikiwamo matokeo ya
vipimo vya madaktari kuhusu afya ya mtoto huyo kabla ya kuchukua hatua
zaidi.
Kamanda Paulo alisema watuhumiwa hao wanashikiliwa kwa kosa la kumfanyiwa mtoto vitendo vya kikatili.
Hata hivyo, kamanda huyo alisema polisi
wanakadiria kwamba mtoto huyo alianza kufichwa kwenye boksi hilo akiwa
na umri wa mwaka mmoja na nusu.
0 comments:
Post a Comment