
KOCHA wa zamani wa Taifa Stars, Mshindo Msolla amesema timu
sumbufu ya Mbeya City inavuna ilichokipanda baada ya kupata mwaliko wa
kushiriki kwenye michuano mipya ya Cecafa Nile Basin yatakayoanza
kutimua vumbi Alhamisi ya wiki hii.
Mbeya City ndiyo wawakilishi wa Tanzania Bara
katika michuano hiyo ya Cecafa inayoshirikisha timu kutoka nchi zilizoko
kwenye bonde la Mto Nile za Kenya, Sudan, Sudan Kusini, Tanzania,
Uganda, Zanzibar, Misri, Ethiopia na Djibouti. Zanzibar itawakilishwa na
timu ya Polisi Zanzibar.
Mbeya City ambayo imepangwa na timu za AFC
Leopards ya Kenya, El Merreikh Al Fasher ya Sudan na Elman ya Somalia
katika kundi B, inashiriki mashindano ya Cecafa kwa mara ya kwanza baada
ya kupanda daraja na kushiriki ligi kuu kwa mara ya kwanza msimu
uliomalizika na kufanikiwa kumaliza katika nafasi ya tatu.
“Nawashauri tu wakapambane na wasiogope majina ya
hizo timu kubwa kwani kama walivyoweza hapa nchini pia nje wataweza,”
alisema Msolla aliyewahi kuifundisha Taifa Stars kabla ya ujio wa
Mbrazil Marcio Maximo.
Kwa upande wake kocha msaidizi wa Mbeya City, Maka
Mwalwisi alisema, “Hii kwetu ni changamoto mpya, tunakwenda kucheza na
timu kubwa na zenye uzoefu wa kimataifa, natumai hiyo ni fursa kwetu
sisi kujifunza zaidi.
“Mbali na kujifunza pia tutakwenda kupambana ili
tuweze kuieperusha bendera ya nchi yetu vyema, kamwe hatutalala na
kupoteza fursa hiyo,” aliongeza Mwalwisi.
0 comments:
Post a Comment