Nyota huyo aliyekuwa akiwania tuzo zaidi ya nne
sambamba na Lady Jaydee, alimgaragaza mshindani wake baada ya kubeba
tuzo zote huku mwanamuziki huyo wa kike akiambulia tuzo mbili za Wimbo
Bora wa Zouk Rhumba na Mwimbaji Bora wa Kike Kizazi Kipya ambazo Diamond
hakushiriki.
Kwa ujumla Diamond alifanikiwa kunyakua tuzo zote
saba alizokuwa akiwania; Wimbo Bora wa Mwaka, Wimbo Bora Wa
Kushirikiana, Wimbo Bora wa Afro Pop, Video Bora ya Muziki ya Mwaka,
Mtumbuizaji Bora wa Kiume, Mtunzi Bora wa Mwaka Kizazi Kipya na Mwimbaji
Bora wa Kiume Kizazi Kipya.
Tuzo hizo zimemfanya mwanamuziki huyo kuvunja
rekodi ya Bendi ya Mashujaa ambayo mwaka jana ilitwaa tuzo tano. Mara ya
mwisho Diamond kutamba katika tuzo hizo ilikuwa mwaka 2012 alipotwaa
tuzo tatu za KTMA.
Staa huyo anasema tuzo alizozipata ni chachu kwake
na anaamini zitazaa matunda katika tuzo za kimataifa anazowania za MTV
Africa maarufu kwa jina la MAMA.
Katika tuzo hizo zinazotarajiwa kutolewa Juni 7,
Diamond anawania vipengele viwili, Mwanamuziki Bora wa Kiume na Kolabo
Bora kupitia ‘Number One’ (Remix) aliyomshirikisha Davido kutoka
Nigeria.
Anasema Watanzania wamethibitisha kwamba yeye anafanya muziki ulio bora hivyo anaamini kwamba ataweza kukubalika pia kimataifa.
“Huu ni utabiri kwangu na kwa Watanzania wote,
kitendo cha kunyakua tuzo zote nilizoteuliwa kinanifanya nijiamini zaidi
katika tuzo za MAMA ambazo Watanzania wengi walishaanza kukata tamaa
kutokana na vigogo niliokaa nao katika vipengele hivyo, ila cha kuamini
ni kwamba tunaweza iwapo tutapiga kura za kutosha,” anasema Diamond.
Washindi wa KTMA 2014
Bendi ya muziki wa Taarab ya Jahazi Morden Taarabu
iling’ara baada ya kutwaa tuzo nne; Kikundi Bora cha Mwaka cha Taarabu,
Mtunzi Bora wa Mwaka Taarabu, Mwimbaji Bora wa Kiume Taarabu (zote
zilikwenda kwa Mzee Yusuph) na Wimbo Bora wa Taarabu.
Isha Ramadhani naye kutoka Mashauzi Classic
alifanikiwa kupata tuzo mbili ikiwamo ya Mwimbaji Bora wa Kike Taarabu
na Mtumbuizaji Bora wa Kike wa Muziki. Fid Q naye aling’ara baada ya
kutwaa tuzo mbili ikiwamo ya Mtunzi Bora wa Mwaka Hiphop na Msanii Bora
wa Hiphop.
Kundi wa Weusi pia lilipata tuzo mbili ikiwamo ya
Wimbo Bora wa Hiphop na Kikundi Bora cha Mwaka cha Kizazi Kipya. Bendi
ya Mashujaa ilifanikiwa kupata tuzo ya Wimbo Bora wa Kiswahili Bendi na
Bendi ya Mwaka.
0 comments:
Post a Comment