KUNA kasheshe moja linanukia kwenye usajili mpya. Ni kasheshe ambalo
Simba huenda wakachekelea kwa vile linaweza kuleta athari kwa watani wao
wa jadi, Yanga. Tayari kocha wa Jangwani, Hans Pluijm, ameshakosa raha
na anakuna kichwa. Kwa mujibu wa azimio la Bagamoyo ambalo
lilikubalika na klabu zote za Ligi Kuu Bara kwamba lianze kutumika msimu
ujao, klabu za ligi hiyo zitalazimika kupunguza idadi ya wachezaji wa
kigeni kutoka watano mpaka watatu. Lakini klabu zitapaswa kukutana
hivi karibuni kupitisha upya makubaliano hayo ambayo kama Shirikisho la
Soka la Tanzania (TFF) likiyakomalia, itakuwa ni hasara kwa Yanga kwani
haitakuwa na nafasi ya kuwachomeka wachezaji wake wawili wa kigeni.
Didier Kavumbagu wa Burundi na Mbuyu Twite wa Rwanda. Wachezaji hao
mikataba yao imemalizika na kufanya Yanga kusaliwa na wachezaji watatu
wa kigeni wenye mikataba ambao ni Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza wote wa
Uganda pamoja na Haruna Niyonzima wa Rwanda. Hatma ya Twite na
Kavumbagu kuongezewa mikataba itategemea na uamuzi wa kikao cha viongozi
wa klabu na TFF kitakachofanyika hivi karibuni kujadiliana mambo
mbalimbali likiwemo hilo la usajili wa wachezaji watano wa kigeni. Pluijm amekiri kwamba bado hajafanya uamuzi kutokana na utata wa idadi ya wachezaji wa kigeni. Simba
huenda isiathirike kama makubaliano hayo yatapita kwani imepanga
kumchomoa kipa Mghana, Yaw Berko kwenye usajili wake na kumsajili kipa
wa Yanga, Ally Mustapha 'Barthez'. Hivyo Simba itakuwa imesaliwa na
wageni watatu ambao ni mabeki Donald Mosoti (Kenya), Joseph Owino
(Uganda) na straika Amissi Tambwe wa Burundi. Azam yenyewe ina
wachezaji wanne wa kigeni, Kipre Tchetche, Kipre Bolou na Mohammed Kone
wote wa Ivory Coast na Brian Umony wa Uganda. Akizungumza hilo,
Kavumbagu aliyemaliza msimu akiwa na mabao 13, alisema: "Mimi siwezi
kukaa muda wote huo nikisubiria kanuni hizo mpya za usajili, kama
wananihitaji wanipe mkataba nisaini, kikubwa wanachotakiwa kutambua kuwa
soka ndiyo ajira yangu. "Nipo tayari kuichezea timu yoyote ile
inayohitaji, hata JKT Ruvu wenyewe wakinihitaji wanifuate kwa ajili ya
mazungumzo kwa masharti maalumu nitakayohitaji kwenye mkataba wangu." Alipoulizwa
kuhusiana na suala hilo, Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa,
alisema: "Klabu zinatakiwa kuwa makini katika kipindi hiki cha usajili
kwa ajili ya msimu ujao, kikubwa zinatakiwa kufuata kanuni za usajili."
0 comments:
Post a Comment