Zawadi za Vodacom ligi ya Bara bado hazitoshi
Mdhamini mkuu wa ligi kuu ya Bara, kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom, imetangaza ongezeko la fungu la zawadi kwa washindi wa msimu uliopita.Katika ongezeko hilo, kwa mfano, bingwa wa ligi kuu ya Bara wa mwaka huu timu Azam itakabidhiwa sh. milioni 75 ikiwa ni ongezeko la sh. nusu milioni kulinganisha na kiasi ilichopata Yanga kwa kunyakua taji hilo mwaka jana.
Ni wazi, tunaamini Nipashe, Vodacom na mshirika wake katika mkataba wa udhamini wa ligi hiyo shirikisho la soka, TFF, walitangaza ongezeko la zawadi hilo mwishoni mwa wiki wakiwa na faraja kubwa mioyoni mwao kwamba limefanyika jambo la maana.
Hatukatai, Nipashe, kwamba zawadi ya sh. milioni 75 kwa bingwa wa ligi kuu ya Bara, kwa mfano, ni fedha nyingi kuliko kiasi kingine chochote ambacho kimewahi kutolewa tangu udhamini wa makampuni -- kwanza bia na baadaye simu -- uingie kwenye michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya klabu nchini.
Lakini sh. milioni 75 hizi, tunafahamu Nipashe pia, ni fedha nyingi kwa sababu ndicho kiasi pekee kilichopo 'mezani' na si kwa thamani ya fedha zenyewe hasa.
Ili kufahamu kwamba sh. milioni 75 ni fedha kidogo kiasi gani katika thamani katika mazingira ya uendeshaji wa timu za ligi ya Bara, unaweza kulinganisha idadi hiyo na wingi wake katika sarafu za kimataifa kama dola za Marekani.
Lakini tutakuwa tunawaonea Vodacom na TFF, Nipashe tunaona, kama thamani ya sh. mlioni 75 za bingwa wa ligi kuu ya Bara tutaiangalia katika uchache wake katika fedha za kigeni peke yake.
Ligi kuu ya Bara si tu ndiyo shindano kubwa zaidi la mchezo wowote nchini kwa sasa, Vodacom na TFF zinatakiwa kutambua, lakini pia ni tukio ambalo linakuwa kwenye midomo, macho na masikio ya walaji kwa karibu mwaka mzima.
Aidha, katika miaka ya karibuni, hasa kutokana na misingi imara iliyowekwa na awamu ya kwanza ya uongozi wa TFF, ligi kuu ya Bara imetokea kuwa michuano yenye thamani zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki kiasi cha kuvutia wachezaji mahiri kutoka ligi nyingine nne za eneo hilo.
Lakini thamani hii, Vodacom na TFF lazima zifahamu, kimsingi imepandishwa si kutokana na jitihada za kutosha za mdhamini na shirikisho la soka hilo.
Na hapa ndipo ambapo mchango wa Vodacom, tunaona Nipashe, ulipaswa kuwa mkubwa hata zaidi ya mara dufu ya udhamini wake wa sasa.
Vodacom na TFF ni lazima zifahamu kuwa ili kuwa katika hadhi ambayo ligi kuu ya Bara ipo na hivyo kuvutiwa kampuni kuwekeza kwayo: timu zenye vikosi kabambe, ushindani wa hali ya juu, viwanja vya kisasa na idadi kubwa ya watazamaji kuliko nchi nyingine yoyote kusini mwa jangwa la Sahara, klabu zimekuwa zikitumia mpaka gharama zilizo nje ya jumla ya mapato yake kwa mwaka kufanikisha hilo.
Na hapa, pengine, ni washindi wa sh. milioni 75 hizo za Vodacom tu ndiyo ambayo huwa haiachi madeni ndani na nje ya klabu katika msimu wa wowote wa ligi kuu ya Bara kutokana na kuwa na muundo wa utawala na mfumo wa kipekee wa uendeshaji kulinganisha klabu nyingine yoyote nchini.
Itakuwa ni makosa, basi, tunaona Nipashe, mdhamini wa ligi hiyo na TFF kujionea fahari mafanikio ambayo yanapatikana kwa 'damu' huku Vodacom ikiwa na uwezo, tunaamini, wa kutoa zaidi kwa mlinganisho na zawadi za ligi kuu nyingine zenye mvuto hata chini ya ile ya Bara kibiashara.
Hatusemi kwamba Vodacom ilipe viwango vya Afrika Kusini, lakini je Vodacom na TFF zinafahamu bingwa wa PSL kwa mfano analipwa kiasi gani? Sh. bilioni 1.5 katika randi.
Achana na timu kama Mbeya City, Kagera Sugar, Coastal Union ama JKT Ruvu. Sh. bilioni 1.5 inaweza kuzifanyia nini Yanga na Simba, kwa mfano?Kufuta madeni yake yote ya msimu mzima.
Na kuna ziada ya motisha ya sh. milioni 227 kwa kila timu ambayo itaongoza ligi baada ya mechi saba kwenye PSL.
Tuchukue furasa hii basi, Nipashe, kuishauri TFF kuona umuhimu wa kuitaka Vodacom kuona umuhimu wa kuongeza kiwango cha udhamini wake kwenye michuano hiyo kwa msimu ujao, hasa katika kipindi ambacho baadhi ya wadhamini wadogo kwenye ligi kuu ya Bara wanatoa mpaka sh. milioni 100 kwa kila timu kwa kushiriki tu.
0 comments:
Post a Comment