Friday, April 18, 2014

SAID NDEMLA: Yanga watakaa chini Jumamosi

 

MSIMU huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara utamalizika keshokutwa Jumamosi ambapo timu zote 14 zitacheza mechi zao za kukunja jamvi huku tayari Azam FC ikiwa imeshatwaa ubingwa.
Azam iliyotinga ligi hiyo kwa mara ya kwanza miaka saba iliyopita, kwa misimu kadhaa nyuma ilihaha kusaka taji hilo na msimu uliopita iliishia kushika nafasi ya pili, lakini safari hii imefanya kweli ikiizidi akili Yanga ambayo ndiyo mshindi wa pili na Simba ambayo msimu huu imepotea njia. Iko nafasi ya nne.
Katika funga dimba ya ligi, mechi kubwa inayosubiriwa na wengi ni ile ya watani wa jadi, Simba na Yanga, itakayochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Ni mechi ya kulinda heshima kwa timu hizo pinzani.
Katika mzunguko wa kwanza, timu hizo zilitoka sare ya mabao 3-3 kwa Simba kufunga mara tatu kipindi cha pili kujikomboa. Desemba mwaka jana zilicheza tena katika mechi ya Nani Mtani Jembe na Simba ikashinda 3-1.
Kwa kawaida mechi ya watani hao huvuta hisia kubwa kuanzia kwa wachezaji, makocha, wanachama na hata mashabiki. Ndivyo ilivyo na mechi hii pia.
Said Ndemla ni kiungo wa Simba ambaye ametamba kuifunga Yanga katika mechi hiyo, lakini akisisitiza zaidi kuwa msimu ujao Simba itakuwa tishio.
Ndemla alisajiliwa na Simba B kwanza akitokea Red Coast ya Mburahati baada ya kushiriki Kombe la Kinesi na kuonwa na watu wa Simba ambayo hufanya mazoezi yake uwanjani hapo, Uwanja wa Kinesi.
“Mechi hii kwa ukweli huwa ni ngumu kutabirika, msimu huu mambo yetu hayajakuwa mazuri, tunajua wanatudharau lakini ukweli ni kwamba lazima Yanga wafungwe pamoja na ubora wao,” anatamba Ndemla.
“Kufanya vibaya kwetu hakumaanishi tutafungwa na Yanga, ni mechi kubwa na tumejipanga kupoza machungu kupitia watani wetu. Yanga ni walewale tuliokutana nao mzunguko wa kwanza na kwenye mechi ya Nani Mtani Jembe, hivyo wajiandae kuchapwa, binafsi hakuna ninayemuhofia Yanga.”
Changamoto binafsi
“Huu ni msimu wangu wa kwanza kucheza Ligi Kuu, nimekumbana na changamoto nyingi, ligi ngumu na ina upinzani mkubwa na niliona ugumu mkubwa wa ligi katika mechi yangu ya kwanza na Yanga,” anasema.
“Nakumbuka mechi ile tulifungana bao 3-3 ambapo walianza kwa kutufunga na tukarudisha zote, niliingia uwanjani nikiwa na wasiwasi mkubwa kucheza na Yanga.

 

0 comments:

Post a Comment

Designed by Adamu Mwanakatwe