INSHALLAH: Bado mechi nne tu!
Kikosi cha Liverpool. LIVERPOOL, ENGLAND
STEVEN Gerrard aliwakusanya wachezaji wenzake huku
machozi yakimtoka baada ya ushindi wa mabao 3-2 wa Liverpool dhidi ya
Manchester City wa juzi Jumapili na kuwaambia: “Inshallah tutachukua
taji.”
Kwa mujibu wa vipaza sauti, Gerrard aliwaambia
wachezaji wenzake wasahau haraka matokeo hayo na kujiandaa kwa ajili ya
mechi ijayo dhidi ya Norwich City wikiendi ijayo.
“Sikilizeni, mechi hii imepita. Tunakwenda
Norwich. Itakuwa hivihivi. Tuko pamoja. Twendeni,” alisikika Gerrard kwa
mujibu wa sauti iliyonaswa na vipaza sauti vya uwanjani Anfield.
Mara baada ya mechi hiyo, nahodha huyo alifanya
mahojiano na waandishi wa habari na kufafanua alichosema huku
akisisitiza: “Nilikuwa na hisia kali, inabidi tuwe watulivu. Kuna mechi
nne zinakuja na mechi hizo zina maana kubwa sana.”
Kuhusu ushindi dhidi ya Manchester City, Gerrard
alisema: “Hilo ndio onyo kubwa tulilotoa mpaka sasa. Tulionyesha kuwa
tunakwenda mpaka mwisho. Hizi ni dakika 90 ndefu zaidi nilizowahi
kucheza katika maisha ya soka. Nilikuwa najiuliza sekunde zinasogea
vipi. Kuna wakati nilidhani sekunde zilikuwa zinarudi nyuma.
“Hata hivyo haya ni matokeo makubwa kwetu. Tuna
mechi nne zilizobaki ambazo kila moja ni kama fainali. Watu wanasema ile
ilikuwa mechi kubwa iliyobaki, nawakatalia, mechi kubwa ni dhidi ya
Norwich City. Tunawaacha wengine wasema kwamba kombe liko mikononi mwa
nani. Wataalamu watasema, lakini hakuna kilicho chetu mpaka sasa.”
0 comments:
Post a Comment