Buriani Kamanda Muhidin Gurumo
Sijui niseme nini, sijui nilie, lakini Napata shaka hakuna
atakayenielewa kwa vijana wengi ambao wamenizunguka hapa nilipo
hawafahamu thamani ya mwanamuziki nguli Muhidin Mwalimu Mohammed Gurumo
maarufu Kamanda, ambaye amefariki dunia.
Sitaki kuamini ninachokisikia kutokana na baraka
nilizozipata kwa nguli huyu, ikiwemo tuzo kwa kuandika makala zake,
kumtambulisha kwa mara nyingine kwenye jamii baada ya kujitambulisha
mwenyewe kupitia muziki wake aliouimba kwa ustadi mkubwa, lakini
heshima, uthamini na kujali alipokuwa akinipa pindi ninapomtembelea
nyumbani kwake.
Lakini sitasahau alipokuwa akifanya mazoezi Jumamosi kadhaa na kuja hadi ofisini kunisalimia.
Mara nyingi alikuwa mcheshi na mwenye utashi,
namnukuu, “Waandishi wengi wamekuwa wakinihoji, lakini Mwananchi mna
utashi mkubwa na mahojiano yenu yanayoendelea nami yananifanya nipate
watu wapya wanaonifahamu na kunikumbuka ambao walinisahau kabisa ikiwemo
Serikali,”alisema Gurumo akinisindikiza kutoka nyumbani kwake Makuburi
hadi kituo cha mabasi cha Gereji, ambako nilipanda gari na kurudi
ofisini.
Binafsi napata ukakasi kuandika makala haya,
lakini nakiri kuwa hakuna jinsi zaidi ya kukubali alichokifanya Mungu
kwa kuwa kazi yake haina makosa, kabla ya kuendelea nasema “Pumzika kwa
amani kipenzi, Muhidini Mwalimu Gurumo.
Namfahamu Gurumo kutokana na kuwa mpenzi wa muziki
wa wa zamani, lakini kukutana naye na kuzungumza naye kirefu ilikuwa ni
mwaka jana, nilipomtembelea nyumbani kwake Ubungo Makuburi, jijini
Dar es Salaam.
Lengo la safari yangu ilikuwa ni kufahamu hali
yake baada ya kupata taarifa za kuumwa kwake na kulazwa katika wodi ya
wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Baada ya kuugua kwa muda mrefu ugonjwa wa moyo na
mapafu, lakini pia nilienda kuchota hazina ya historia ya maisha yake ya
muziki.
Gurumo alikuwa mcheshi na mwenye moyo wa kunifahamisha yeye ni nani na alitoka wapi na anafahamu nini kuhusu muziki wa dansi.
Nikiwa kwake, tulizungumza mambo mengi ambayo
yalinifanya niandike makala kadhaa za kuvutia kumuhusu mwanamuziki huyu
nguli, moja ya malalamiko yake ilikuwa ni kuimba muziki kwa miaka kadhaa
bila mafanikio, lakini akanidokeza lengo lake la kustaafu muziki
kutokana na afya yake kutokuwa nzuri na umri kuwa mkubwa.
Gurumo (74), alitangaza uamuzi wake wa kustaafu
muziki Agosti 22, mwaka 2013 , alipozungumza na waandishi wa habari
kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo), jijini Dar es Salaam.
Wakati huo alizungumza mambo mengi na mojawapo ni
kustaafu muziki bila kuwa na kitu chochote cha maana hata baiskeli licha
ya kuimba kwa zaidi ya miaka 50.
0 comments:
Post a Comment