Monday, April 28, 2014

Ryan Giggs awarudisha pamoja Man United

JUZI Jumamosi, makocha wawili walioingia uwanjani Old Trafford kupambana kila mmoja akiwa na yake kichwani. Neil Adams wa Norwich City alikuwa anawaza jinsi ya kukwepa kushuka daraja, Ryan Giggs alikuwa na presha ya mwanzo wake utakuwaje klabuni Manchester United baada ya kutajwa kuwa kocha wa muda.
Hata hivyo, hadi kufika mwisho wa dakika 90, mechi ilikuwa ya upande mmoja na kocha mpya alianza vyema kibarua chake Old Trafford.
Pengine ameweza kuiongoza Man United kwa mechi moja tu dhidi ya Norwich, lakini Giggs alitimiza ahadi ya kurudisha upya makali ya Man United ambayo msimu huu wamefungwa na Stoke City, West Brom, Swansea, Everton na Sunderland baada ya kushinda 4-0 na kumfanya mpinzani wake Neil Adams akiwa kwenye hofu kubwa ya kushuka daraja.
Wakati Giggs akiwa anapita kwenye korido za Old Trafford kuelekea uwanjani kabla ya mechi kuanza, zaidi ya mashabiki 70,000 walilipuka shangwe kumshangilia shujaa wao wakimsapoti baada ya kupewa kibarua cha kuinoa timu yao. Old Trafford iliungana tena.
Kwenye rekodi yake ya kucheza mechi 962 alizochezea Man United, Giggs amekuwa mchezaji mwenye hadhi kubwa sana kwenye klabu hiyo kwa karibu miongo miwili yenye mafanikio na anaendeleza mafanikio. Kwenye mechi yake ya kwanza kama kocha, hata kama ni kwa muda tu zimekuja kwenye nyakati ambayo Man United ipo pabaya Ligi Kuu England.
Giggs, 40, Jumanne iliyopita alichaguliwa kuwa kocha wa muda baada ya David Moyes kutimuliwa, ikiwa ni miezi 10 tu tangu alipomrithi Sir Alex Ferguson. Kwenye mchezo huo, mashabiki walidiriki hata kubeba mabango ya kumsifu Giggs na wakidai ndiye hasa chaguo spesho na si Moyes.
Giggs ni chaguo la wengi katika kuongoza Man United hadi mwisho wa msimu. Katika kuonyesha miezi 10 ya Moyes klabuni imashasahaulika, bango lake la ‘The Chosen One’ lililokuwa limewekwa kwenye jukwaa la Stretford End uwanjani Old Trafford tangu Agosti mwaka jana liliondolewa mapema sana saa chache tu baada ya kufutwa kazi. Giggs amerudisha sherehe tena Old Trafford. Man United imeungana tena.
Giggs alipokuwa anaelekea kwenye kiti chake alionekana kuwa ni kocha wa haja. Alivaa suti na tai yake vizur na alikuwa akishangiliwa muda wote na mashabiki wa Man United. Alipata muda pia wa kusaini vitabu vya mashabiki hao.
Ilikuwa rahisi kuona Man United waliamua kuwa pamoja kumsapoti shujaa wao aliyekuwa nao pamoja kwa miaka yote waliyotwaa mataji 13 ya Ligi Kuu England kwenye mazingira kama hayo ya burudani kubwa. Lakini, kwa msimu huu mambo yametibuka, klabu hiyo itamaliza ligi ikiwa na pointi chache zaidi kwenye historia yao kwenye ligi hiyo. Hakuna mataji msimu huu na watakosa michuano ya Ulaya msimu ujao.
Kudhihirisha kwamba wameungana tena kwa pamoja bila ya kujali hatatwaa ubingwa msimu huu na msimu ujao watakosa Ligi ya Mabingwa Ulaya, mashabiki walipeperusha bendera uwanjani Old Trafford na nyimbo za ushindi ziliimbwa kuonyesha umoja umerudi ‘Theatre of Dreams’ na kuamini kwamba sasa wanaelekea kwenye kuupa kisogo wakati mgumu klabuni hapo.
Kabla haya ya mechi hali ilionekana kubadilika klabuni hapo. Giggs aliahidi kurudisha tabasamu kwenye vyuso za mashabiki na timu ilicheza kwenye ‘mfumo wa United’ na kwa hilo Giggs alitimiza ahadi yake kwa haraka sana.
Kundi la mashabiki walisikika wakiimba nyimbo za “United imerudi” hasa baada ya kuonekana kucheza kwa moyo kama ilivyokuwa enzi za Sir Alex Ferguson. Kwa kuanzia si kitu kibaya na Giggs alionyesha ishara nzuri na kuwaunganisha pamoja Man United ambao walionekana kusambaratika kwenye kipindi cha Moyes

 

0 comments:

Post a Comment

Designed by Adamu Mwanakatwe