Mzee aliyekatwa nyeti asimulia mkasa mzima
Mzee London Haonga akihojiwa na Brandy Nelson katika hospitali ya rufaa jijini Mbeya
Mbeya. Aprili 19, Mzee London Haonga (61) alipatwa na tukio la
kutisha kwa kukatwa sehemu zake za siri. Ni tukio la kusikitisha ambalo
linadaiwa kufanywa na vijana wadogo.
Haonga alipatwa na masahibu hayo akiwa nyumbani
kwake Kijiji cha Mapogolo wilayani Ileje. Majirani walisikia yowe kutoka
kwa mzee huyo na kufika eneo la tukio, lakini walikuwa wamechelewa kwa
kuwa wahalifu hao walikuwa tayari wameshatokomea na viungo vya siri kwa
mzee huyo.
Hata hivyo, majirani hao walimbeba mzee huyo hadi
Hospitali ya Wilaya ya Ileje ambako alihamishia Hospitali ya Rufaa Mbeya
alikolazwa mpaka sasa.
Akizungumza na gazeti hili akiwa Wodi 1, Haonga
anasema tukio hilo kwake lilikuwa la kinyama na ukatili kwani wahusika
walimchinja bila huruma na kumsababishia maumivu makali ambayo
yalisababisha apoteze fahamu.
“Ilikuwa Jumamosi saa 8.00 mchana alipokuja mjukuu
wa kaka yangu nyumbani kwangu na kunieleza kuwa alitumwa kuja kuchukua
dawa ya kizunguzungu. Nilimjibu kuwa sina dawa hiyo hapa ndani hadi
niende kutafuta porini. Hivyo tukakubaliana kuwa atakuja jioni kuchukua
dawa,” anasema mzee huyo ambaye ni mtaalamu wa dawa za asili.
Anasimulia kuwa ilipofika saa 2:30 usiku alifika
kijana huyo na akampa dawa hiyo. Alipotaka kuondoka alimwomba
amsindikize na akampa fimbo kwa ajili ya kujilinda njiani kwa kuwa nje
kulikuwa na giza nene.
“Tulipotoka nyumbani, tukiwa mbali kidogo na
nyumbani kwangu, ghafla akanifunika usoni na kofia aliyokuwa amevaa na
kunikaba shingo huku akiniambia kuwa ‘Wewe mzee leo utaona,’ baadaye
akaniangusha chini,” anasema.
Akisimulia huku akionyesha kujisikia maumivu
makali, Haonga anasema baada ya kuanguka chini, aligundua kuwa mjukuu
wake hakuwa peke yake.
“Walikuwa zaidi ya watu wawili kwa kuwa nikiwa
nimezibwa uso na kofia na kukabwa shingo, mwingine alinimvua suruali,”
anakumbuka.
Anasema kuwa baada ya muda mfupi alipoteza fahamu
na alizinduka akiwa wodini Hospitali ya Rufaa na kuelezwa na wauguzi na
madaktari kuwa sehemu zake za siri zimeondolewa na kubakia kidonda
ambacho anaendelea kupatiwa matibabu.
Mzee Haonga anasema kuwa bado hali yake siyo nzuri
kwani maumivu anayoyapata ni makali na kwamba maumivu mengine anayapata
katika sehemu ya shingo na kifua.
Anasema kuwa nyumbani kwake anaishi peke yake
katika kipindi cha miaka minne kutokana na kufiwa na wake zake wawili na
kubakiwa na watoto ambao wote wanajitegemea, hivyo anaamini watu hao
walitumia nafasi hiyo ya kumlaghai na kumfanyia unyama huo .
0 comments:
Post a Comment