Monday, April 28, 2014

Chelsea yatia nazi supu ya Liverpool, yaiangusha kichapo kwao Anfield

 

Straika wa Chelsea, Demba Ba akipita na mpira katikati ya viungo wa Liverpool, Lucas (kulia) na Steven Gerrard (kushoto) wakati wa mchezo wa Ligi Kuu England uliofanyika Anfield jana Jumapili. Chelsea ilishinda 2-0.  

MAMBO si mambo Anfield, Chelsea imetia nazi supu ya Liverpool na sasa imekuwa si supu tena, bali umekuwa mchuzi. Hiyo ni baada ya jana Jumapili kuwachapa mabao 2-0 kwenye Ligi Kuu England na kuwatibulia wenyeji hao kasi yao kuelekea ubingwa wa ligi hiyo.
Bao la straika Msenegal, Demba Ba, kwenye kipindi cha kwanza na jingine la Mbrazili Willian kwenye dakika za lala salama, yalitosha kwa Jose Mourinho na kikosi chake cha Chelsea kuilaza Liverpool kwao na kuwatibulia sherehe zao kuhusu ubingwa ambazo tayari zilikuwa zimeanza Liverpool.
Kwa matokeo hayo, Liverpool sasa inamtihani na kushinda mechi zake zote mbili zilizobaki, huku ikiomba dua mbaya kwa Manchester City ambayo bado ina mchezo mmoja mkononi.
Man City baadaye jana ilitarajia kumenyana ugenini kwa Crystal Palace. Msimamo ulivyo kwa sasa, Liverpool, Chelsea na Man City yoyote inaweza kuwa bingwa.
Kosa la kiungo na nahodha wa Liverpool, Steven Gerrard, liliigharimu timu yake kwenye kipindi cha kwanza alipomruhusu Ba kufunga, kabla ya kupigwa kwa shambulizi la kushitukiza la pasi za kugongeana kati ya Fernando Torres na Willian na hivyo Mourinho kuondoka Anfield na pointi zote tatu.
Kwenye mchezo huo, Mourinho alimzidi mbinu mpinzani wake, Brendan Rodgers kwa kupaki basi muda wote na kushambulia kwa kushitukiza.
Mchezo mwingine wa ligi hiyo uliochezwa jana Jumapili, Sunderland iliichapa Cardiff City mabao 4-0 na hivyo kuendeleza vyema kampeni yao ya kujinasua kutoka kwenye hatari ya kushuka daraja.

0 comments:

Post a Comment

Designed by Adamu Mwanakatwe