Mabadiliko ya barabara Dar kuanza leo
Mabadiliko makubwa yanafanywa katika Barabara za
Samora na Sokoine. Barabara ya Samora sasa itakuwa inatoka badala ya
kuingia katikati ya jiji kama ilivyokuwa na ile ya Sokoine itakuwa
inaingia tu badala ya kuingia na kutoka katikati ya jiji.
Akizungumzia mabadiliko hayo Meneja wa Barabara za
Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), Mohamed Kuganda alisema kutakuwa
na askari wa usalama barabarani katika maeneo hayo ili kuwaongoza
watumiaji.
Kuganda alisema lengo la mabadiliko hayo ni
kupunguza msongamano wa magari na kuwaandaa wananchi katika mabadiliko
mengine madogo yatakayofuata baadaye mradi wa BRT utakapoanza kazi
rasmi.
Mhandisi huyo alisema baada ya kukamilika kwa
mradi wa mabasi yaendayo haraka, daladala zote zinazotumia Barabara ya
Morogoro hazitaruhusiwa kufika katikati ya jiji, badala yake mabasi
yaendayo haraka yatafanya kazi hiyo.
Mabasi yatumiayo barabara za Kilwa na Ali Hassan
Mwinyi yataendelea kufika katikati ya jiji hata baada ya mradi wa BRT
kukakamilika kwa sababu barabara hizo hazina mabasi yaendayo haraka.
“Pia, daladala zote zinazotoka Mnazi Mmoja kwenda
Posta, hazitaruhusiwa tena kufika Posta Mpya, badala yake zitatumia
Barabara ya Uhuru na kuishia kituo cha Stesheni na kurudi kupitia
Barabara ya Samora,” alisema.
Meneja wa Malalamiko ya Waathirika wa Mabadiliko
wa Wakala wa Usafiri wa Haraka (Dart), Deus Mutasingwa alisema Wakala wa
Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), unashirikiana kwa karibu na wadau
wengine kama Sumatra, Manispaa ya Ilala, trafiki na Wizara ya Ujenzi
katika kuhakikisha shughuli hiyo inafanyika kwa ufanisi.
Mutasingwa alisema wanatarajia kupokea malalamiko
mbalimbali kutoka kwa wananchi kwa sababu jambo hilo ni geni na
litaonekana kuleta usumbufu.
Aliwataka watumiaji wote wa barabara kuwa makini katika kufuata alama za barabarani au mwongozo utakaotolewa.
Mabadiliko yaliyofanyika, pia yanahusisha mabasi
yote yanayopita Barabara ya Kilwa ambayo yataishia Stesheni na kurudi
kupitia njia hiyohiyo.
Mabasi yanayopita Barabara ya Nyerere na Uhuru
yataishia Kituo cha Mnazi Mmoja na kurudi kupitia njia zao. Pia kutakuwa
na mabasi yatakayoanzia Mnazi Mmoja kupitia Bibi Titi, Maktaba hadi
Posta ya Zamani - Benki ya NBC na kurudi kupitia njia hiyohiyo. Mabasi
yote yanayopita Barabara ya Ali Hassan Mwinyi kwenda katikati ya jiji
yataishia katika Kituo cha YMCA Barabara ya Upanga na kurudi kupitia
njia hiyo.
0 comments:
Post a Comment