Monday, April 28, 2014

Kingunge atoboa siri ya Katiba Mpya

                     

Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru, ametoboa siri ya Katiba mpya kuwa ni ile iliyo bora itakayoondoa umaskini wa wananchi na kuwataka wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutengeneza Katiba kwa njia ya maridhiano.


Aidha, mwanansiasa huyo amekerwa na kauli zisizo staha dhidi ya waasisi wa Muungano, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume na za kejeli dhidi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kuratibu maoni ya wananchi kuhusu Katiba mpya, Jaji Joseph Warioba na wajumbe wake.

Akitoa maoni yake kuhusu Rasimu ya Katiba, sura ya kwanza na ya sita bungeni jana, Ngombale Mwiru, alisema wajumbe wanatakiwa kukaa pamoja na kujadili kwa umakini mkubwa rasimu iliyopo mbele yao ili kupata Katiba bora na yenye kubeba maslahi ya wananchi.

“Wananchi wanataka Katiba bora si bora Katiba. Katiba bora ni ile itakayodumisha amani, umoja na mshikamano, Katiba itakayopunguza au kuondoa kabisa mapungufu yaliopo kwenye Muungano.”

“Kero kubwa ya wananchi katika nchi hii ni umaskini tena wakati mwingine uliokithiri, Katiba lazima iboreshe maisha ya watu wanaotegemea mlo moja kwa siku na hata wale wanaotumia zaidi ya dola moja kwa siku bado ni maskini… lazima Katiba kama isiyoboresha haya haifai” alisema.

Aidha, alikosoa hatua ya wajumbe wa Bunge hilo wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususa, akisema inawakosesha fursa ya kutoa maoni yao na kuwataka kufikiria upya uamuzi huo na kurejea bungeni kwa maslahi ya wananchi.

“Kupata Katiba bora lazima kuwe na maelewano, waliotoka wamewakosea wananchi warudi tutengeneze Katiba, hata wakirudi kunatakiwa maelewano ili kupata theluthi mbili ya kura kwa Tanzania Bara na theluthi mbili kwa Zanzibar” alisema na kuongeza:

Aidha, alisema amesikitishwa na lugha zisizo na staha zilizotolewa na baadhi ya wajumbe dhidi ya waasisi wa Muungano, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume. “Waasisi wamedhalilishwa, kuna mmoja alisema Nyerere si Mungu kwani kuna mtu alimwambia ni Mungu?” alihoji.

Alisema amesikitishwa na kauli za kejeli zilizotolewa dhidi ya Jaji Warioba. “Hapa tunapishana mawazo na kupingana kwa hoja…hata rasimu hii ni mawazo tu, hatumzungumzii Warioba wala wajumbe, tunazungumzia rasimu, si busara kumshambulia Warioba au mjumbe yoyote binafsi” alisema.

Ngombale Mwiru pia alitoa ufafanuzi juu ya ushiriki wake katika Bunge Maalum la Katiba, akisema jina lake lilipendekezwa kwa Rais na Baraza la Waganga wa jadi ambalo ni mlezi wake tangu mwaka 1998 na si kuchomekwa kimezengwe kama baadhi ya watu wanavyofikiri.

Akihitimisha mjadala huo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni wa kipekee duniani kwani umeundwa katika misingi ya udugu wa karibu, hivyo unapaswa kulindwa kwa nguvu zote.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni ya Bunge Maalum la Katiba, Pandu Amiri Kificho, alikanusha madai kuwa amependekeza muundo wa muungano wa serikali tatu, akisema siku zote msimamo wake ni muundo wa serikali mbili ulioboreshwa.

Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Iddi, alisema pamoja na serikali kutumia fedha nyingi kwa ajili ya Bunge hilo, lakini hakuna mafanikio makubwa yaliyopatikana na kuwasihi Ukawa kurudi bungeni kushirikiana na wenzao kutengeneza Katiba bora ya wananchi kwani haitatengenezwa barabarani wala kwenye mikutano ya hadhara.

Bunge Maalum la Katiba liliahirishwa jana hadi Agosti 5, mwaka huu.

0 comments:

Post a Comment

Designed by Adamu Mwanakatwe