Maaskofu 32 Katoliki wataka Tume ya Warioba iheshimiwe
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar, Augustino Shao akiwasha Mshumaa wa Pasaka wakati wa Misa ya mkesha wa Pasaka uliofanyika kwenye Kanisa la Kuu la Makatifu Joseph, Zanzibar jana. Picha na Martin Kabemba
Dar es Salaam. Maaskofu 32 wa
Kanisa Katoliki Tanzania, wametoa waraka maalumu wa Pasaka wakiwataka
wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuheshimu maoni ya Watanzania
yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na kuweka pembeni itikadi za kisiasa
katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya.
Kupitia tamko lao la pamoja walilolitoa jana na
kulipa jina la “Ujumbe wa kichungaji wa Pasaka kwa waamini na watu wote
wenye mapenzi mema,” maaskofu hao walisema hivi sasa kuna makundi yenye
nguvu ambayo yameanza kushinikiza kuingizwa mambo yenye masilahi kwao
kwenye Katiba Mpya.
“Tunalisihi na kulishauri Bunge Maalumu la Katiba
kuheshimu mawazo yaliyowasilishwa na kutumia busara zilizopendekezwa za
kujenga muundo wa Muungano utakaokidhi mahitaji ya utangamano,
mshikamano, amani, maadili, uhuru na uwajibikaji wa viongozi na raia wa
Tanzania,” walisema katika tamko hilo ambalo, Makamu wa Rais wa TEC,
Askofu Severine Niwemugizi alithibitisha kuwa umetolewa na kanisa hilo.
Kauli ya viongozi hao ambayo ilisomwa katika
makanisa mbalimbali nchini jana, imekuja ikiwa zimepita siku sita tangu
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia vikao vya Bunge Maalumu la
Katiba kutokana na mvutano unaoendelea juu ya hoja ya muundo wa
Serikali.
Tangu kuanza kwa Bunge hilo kumekuwa na mvutano
kuhusu muundo wa Serikali, huku CCM kikiupinga muundo wa serikali tatu
uliopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kutaka muundo wa
serikali mbili, ambao unapingwa na upinzani.
“Kazi ya kuandika Katiba ni ngumu na haishangazi
kuona migongano ya hoja kwa makundi kinzani. Mawazo ya wengi
yamewasilishwa kisheria na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa ajili ya
kujadiliwa na Bunge Maalumu la Katiba,” inasomeka sehemu ya tamko hilo
ambalo limechapishwa kwa ukamilifu katika ukurasa wa 6 wa gazeti hili na
kuongeza:
“Sasa, tunashuhudia makundi yenye nguvu yakijaribu
kushinikiza kuingizwa matakwa yake kwenye Katiba kwa njia zozote zile
ili kujihakikishia kuendelea kulinda masilahi yake ya kisiasa.”
Maaskofu hao ambao majina yao yameorodheshwa
kwenye waraka huo, wamewataka wajumbe wa Bunge hilo kuachana na itikadi
za kisiasa ili kufikia mwafaka katika masuala muhimu
yatakayowahakikishia raia wa kawaida kushiriki kwenye fursa za maendeleo
kwa manufaa ya wote.
Huku wakitolea mfano umoja, amani na utulivu
nchini ambao umekuwa kimbilio kwa mataifa mengine, walisema hivi sasa
kuna dosari kadhaa katika umoja wa Watanzania.
“Kupungua kwa hisia za kujisikia watu wote ni
taifa moja, ni dosari iliyoanza kukua taratibu na sasa inaonekana kuwa
ndiyo ukweli,” walisema.
Walisema kasoro zilizojitokeza katika mambo
mbalimbali ndiyo chanzo cha watu kutaka mabadiliko: “Watu wengi walitaka
na wanataka mabadiliko au mageuzi ya msingi. Kwa msukumo huo ndiyo
sababu ya kuingia katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya.”
0 comments:
Post a Comment