KUTOKA LONDON: Athari za anguko la Manchester United
LIGI Kuu England inaelekea ukingoni na ndoto
za mabingwa watetezi, Manchester United za kuendelea kubaki na kombe
hilo zimepeperuka baada ya kushuhudia vipigo vingi, hasa nyumbani kwao,
Old Trafford.
Huu ni uwanja ambao katika miaka mingi ya kocha
Sir Alex Ferguson ilikuwa ngome inayoogopwa na wachezaji na makocha wa
timu pinzani, lakini tangu msimu huu umeanza wakiwa chini ya David
Moyes, mambo yamegeuka.
Man United imekuwa timu ya kubezwa, ambayo
imefungwa na timu nyingi ndogo, baadhi ikiwa ni mara ya kwanza katika
historia zao kuwafunga Mashetani Wekundu, mfano Swansea.
Rekodi nyingi zimewekwa na kuvunjwa, lakini kwa
upande hasi kwa United ambao sasa wanajaribu kujitutumua ili walau
wacheze Ligi ya Europa japokuwa vigingi mbele yao bado ni vingi kwa
jinsi timu nyingine zinavyowawekea kauzibe.
Athari za matokeo hayo kisaikolojia zinamuumiza
zaidi kocha ambaye aliona ni heshima kubwa sana kupata nafasi ya
kuwafundisha mabingwa hao na moja ya klabu zinazoheshimika zaidi
duniani.
Lakini matokeo haya naathiri pia chapa ya Ligi Kuu
ya England (EPL) machoni pa ulimwengu wa michezo, kwa sababu kimsingi
kutetereka huko kunashusha kwa namna fulani hadhi ya ligi yenyewe.
Hii ni kwa sababu za anguko la Manchester United
haziishii ndani tu, bali pia nje ya nchi, kwa sababu kwa mfano kwenye
Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) licha ya kufika hatua ya robo fainali,
ilikuwa bahati zaidi kuliko uwezo.
Tunakumbuka bado jinsi Olympiakos walivyowaadhiri
kwenye mchezo wa kwanza na kuwafunga 2-0, timu ambayo ni ndogo
ikilinganishwa na United. Lakini pia mchezo dhidi ya Bayern Munich
ambapo United walilazimisha sare, ‘waliegesha basi’ ndiyo maana winga wa
Wajerumani hao, Arjen Robben akasema ilikuwa kana kwamba United
wanajihami kwenye mpira wa mikono.
Mtaalamu wa masuala ya soka na biashara kuhusiana
na chapa na matangazo, Evans Brighton anasema kwamba hii ni sawa na
panga lenye kukata kuwili kwa sababu klabu kubwa kama hii inapoanza
kufanya mambo ya ovyo, inapunguza washabiki kwenye ligi husika na
kidogokidogo mapato.
Hii ni timu iliyopata kutwaa ubingwa wa England
mara 20, ikawa na kocha aliyesifika kote duniani na kuna watu waliokuwa
wakiweka fedha zao kwenye ligi hii kwa sababu ya timu, kocha wake, aina
ya wachezaji waliopo au hata wamiliki kwa maana ya uhakika wa kufanya
vyema.
Lakini moja ya klabu kubwa kama hii inapodondoka
tafsiri yake kimataifa ni kwamba na utamu wa ligi unaweza pia kuwa na
tatizo, watu wakaamua kuelekeza macho yao kwenye ligi nyingine.
Ikumbukwe kwamba Ligi Kuu England ndiyo sasa
maarufu zaidi kote duniani, lakini kadiri miaka inavyokwenda watu
wanakuja na hoja kinzani, wakianza kutupia macho Bundesliga (Ligi Kuu
Ujerumani), La Liga (Ligi Kuu Hispania) na hata Ligue 1 (Ligi Kuu
Ufaransa)
0 comments:
Post a Comment