STERLING: Mjamaica aliyeanza kuikamata England
Raheem Sterling akishangilia bao na straika wa LiverpoolSuarez
HAKUNA
unachoweza kubisha. Huu ni wakati wa mwanasoka, Raheem Sterling,
kutamba katika Ligi Kuu England. Ameingilia kombinesheni ya Luis Suarez
na Dan Sturridge na sasa anang’ara kuliko zamani. Jikumbushe kuhusu
uwepo wake Anfield. Ni nani huyu Sterling?
Azaliwa Jamaica, akulia England
Raheem Shaquille Sterling alizaliwa Desemba 8,
1994 katika mji mkuu wa Jamaica, Kingston. Sterling alikulia katika eneo
la Maverley jijini Kingston huku akilelewa na bibi yake. Akiwa na umri
wa miaka mitano alihamia London, England pamoja na mama yake.
Alianza maisha yake ya soka la utotoni katika
klabu ya Queens Park Rangers, lakini Februari 2010 kocha wa wakati huo
wa Liverpool, Rafael Benitez, alimnunua kwa ada ya Pauni 600,000 ambayo
ilitazamiwa kupanda hadi Pauni 5 milioni kutegemea na jinsi ambavyo
angepiga soka lake kwa uhakika Liverpool.
Alicheza mechi yake ya kwanza ya timu ya wakubwa
katika mechi za maandalizi ya msimu dhidi ya Borussia Monchengladbach ya
Ujerumani Agosti Mosi, 2010.
Hata hivyo wakati huo alikuwa bado akiendelea
kutisha katika timu ya vijana kutokana na kasi yake huku akifunga katika
mechi za vijana za Hibernian, Aston Villa na kisha katika michuano ya
FA dhidi ya Notts County. Februari 14, 2011, Sterling alifunga mabao
matano peke yake katika ushindi wa 9–0 dhidi ya Southend United.
Aweka rekodi Anfield
Machi 24, 2012, Sterling aliingia katika pambano
dhidi ya Wigan Athletic akiwa na umri wa miaka 17 na siku 107. Kwa
kufanya hivyo akawa mchezaji wa pili kinda zaidi kuichezea klabu hiyo.
Akacheza tena katika mechi dhidi ya Fulham, kisha katika mechi ya mwisho
dhidi ya Chelsea akiingia katika kipindi cha pili ambapo walishinda
4–1.
Agosti 2012 alicheza mechi yake ya kwanza ya Ulaya
dhidi ya Gomel wakishinda bao moja. Akafunga bao lake la kwanza timu ya
wakubwa katika mechi dhidi ya Bayer Leverkusen katika pambano la
kirafiki.
Alianza mechi yake ya kwanza ya Ligi pale Anfield
siku tatu baadaye katika sare ya 2–2 dhidi ya Manchester City. Akacheza
dakika zote 90 katika kichapo dhidi ya Arsenal Septemba 2 kabla ya
kucheza katika sare dhidi ya Sunderland ambapo alipachikwa kuwa Mchezaji
Bora wa mechi.
Akasafiri kwenda Europa kucheza dhidi ya Young
Boys ya Uswisi akiingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Stewart
Downing katika ushindi wa 5–3 wa Liverpool. Bao la kwanza la Sterling
lilikuja katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Reading. Kwa kufanya hivyo
aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa pili kinda zaidi kuifungia Liverpool
nyuma ya Michael Owen.
Desemba 21, 2012, Sterling alisaini mkataba mpya
na Liverpool. Akafunga bao lake la pili Anfield dhidi ya Sunderland
katika ushindi wa 3-0 akinyanyua mpira juu kwa kipa wao wa sasa, Simon
Mignolet.
0 comments:
Post a Comment