Hakuna Manchester City bila ya mtu huyu
Yaya Toure
KUNA kitu unakiona halafu unashusha pumzi. Ndege inatua, ipo
katika kasi, rubani anaituliza, halafu dakika chache baadaye inasimama.
Unashusha pumzi. Unatafuta mzigo wako ulipo. Ni kama ilivyo unapokuwa
kwenye basi au boti.
Ni kama unavyomalizia kusoma mstari wa mwisho wa
kitabu cha Sidney Sheldon, James Hadley Chase au John Grisham. Unavuta
pumzi na kufunga kitabu huku unatafakari. Ni kama unavyomaliza kutazama
filamu ya ‘Sometimes In April’ inayoelezea mauaji ya Rwanda ya mwaka
1994.
Ni kama nilivyotazama shuti la Yaya Toure dhidi ya
kipa wa Sunderland, Victor Manonne, Jumapili jioni. Akiwa umbali wa
mita 30, alijikunja kiurahisi kama mzaha. Akajikunjua na kuusafirisha
mpira mpaka katika kona ya nyavu ya lango lile la Uwanja wa Wembley.
Hakuna kingine unachoweza kufanya. Unashusha
pumzi. Binafsi nilishusha pumzi na kutafuta albamu yangu ilipo.
Nikatazama picha ambayo nilipiga naye Abidjan Juni 2010. Moyoni
nikajisemea ‘Asante Mungu nilikutana na huyu mtu aliyepiga hili shuti na
nikazungumza naye’.
Ndiyo Yaya Toure, katika ubora wake wa hali ya juu
kabisa kwa sasa ni viungo wachache wanaomudu nguvu zake na akili yake
ya soka. Nilikutana naye katika ardhi ya kwao akiwa hana makeke, mpole
na msikivu aliyepindukia.
Muda mwingi alionekana kusifia ubora wa
mshambuliaji wa Tanzania, Mbwana Samata. Kisha akasifia Taifa Stars
ilivyobadilika, tofauti na ile waliyocheza nayo mechi ya kirafiki
Januari 2010.
Kinachonifurahisha kwa sasa ni jinsi ambavyo
matajiri wa Kiarabu na mashabiki wazungu wa Manchester City hawaiamini
timu yao bila ya yeye. Hakuna Manchester City bila ya Yaya Toure. Sahau
kuhusu, Kun Aguero, David Silva, Alvaro Negredo na wengineo. Hakuna Man
City bila huyu mtu.
Kundi la wachezaji wa Manchester City
linapomzunguka kumpa heshima mtu mweusi anayewabeba, basi ni tukio
ambalo linaweza kutingisha hata kaburi la Martin Luther King. Ni tukio
ambalo linanikumbusha Oktoba 1999 wakati Nwankwo Kanu alipoifunga
Chelsea ‘Hat Trick’ katika dimba la Stamford Bridge na mwisho wa mechi
wazungu; Dennis Bergkamp na Marc Overmas, wakampelekea taulo ajifute
jasho.
Kuna mambo makuu matatu yanayonikosha kuhusu Yaya.
Kwanza kabisa ni Mwafrika ambaye hana makeke licha ya mabilioni ya pesa
anayokamata. Wanasoka wengi wa Afrika ni mabingwa wa matanuzi baada ya
kupokea mishahara mikubwa.
Yaya anapokea Pauni 250,000 kwa wiki. Huwezi
kusikia kuwa amenunua gari la kifahari kupindukia, hauwezi kusikia
amekodi ndege binafsi kwa ajili ya kwenda likizo Abidjan na wala hauwezi
kusikia amenunua saa ya Pauni 2,000.
Lakini jaribu kuangalia makeke ya Emmanuel
Adebayor katika maisha yake ya kila siku halafu mlinganishe na Yaya. Kwa
sasa Adebayor naye anamiliki ndege yake binafsi kwa ajili ya matanuzi.
Usije kudhani kwamba Yaya anaweza kufanya hivyo.
Daniel Amokachi ‘The Bull’ pia akiwa anacheza
Uturuki tu katika klabu ya Besiktas, alinunua ndege ndogo. Sasa anajuta.
Hata Samuel Eto’o Fills naye anamiliki ndege ndogo. Ndivyo wachezaji
wetu wa Kiafrika wanachofikiria kwa haraka zaidi.
0 comments:
Post a Comment