Matajiri Yanga wavamia kambi ya Al-Ahly Cairo
Wachezaji wa timu ya Yanga wakishangilia ushindi wa bao moja dhidi ya timu ya Al-Ahly ya Misri.
MATAJIRI wawili wenye ushawishi mkubwa na wanaofanya mambo mengi
ya Yanga, hawajaridhika na ushindi wa juzi Jumamosi wa bao 1-0 dhidi ya
Al Ahly na sasa wameamua kuivalia njuga klabu hiyo ya Misri kwa kuvamia
mji wao wa Cairo ili kuweka mambo sawa kabla ya mechi ya marudiano ya
Jumapili.
Wakati jopo la Yanga lilitangulia kuwasili Cairo
jana Jumapili kudhibiti mbinu za Waarabu hao na kuhakikisha hakuna
fitna yoyote itakayofanyika, wenyeji wao walikuwa nchini ambapo jioni
walifanya mazoezi yao ya mwisho na baadaye kula chakula cha usiku na
maofisa wa ubalozi wao nchini na wataondoka leo Jumatatu.
Matajiri hao ambao ni Mwenyekiti wa Kamati ya
Mashindano ya Yanga, Abdallah Binkleb na Mwenyekiti wa Kamati ya
Mashindano ya Kimataifa, Seif Ahmed wamewaongoza wanachama wengine
kuingia msituni kuidhibiti Ahly kwa ushirikiano na Watanzania wanaoishi
jijini Cairo, Misri.
Seif aliondoka nchini kimyakimya na akaliambia
Mwanaspoti kwamba wamepania kuiondosha Ahly na wanachokwenda kufanya ni
kuhakikisha Wachezaji wa Yanga wanakuwa chini ya uangalizi mkali katika
kila dakika tangu watakapotua kwenye Uwanja wa Ndege Alhamisi wiki hii.
Seif alisisitiza kuwa walishaanza kuweka mazingira
mapema, lakini sasa wanakwenda kujidhatiti zaidi kuanzia kwenye Uwanja
wa kufanyia mazoezi, hoteli, mabasi pamoja na vyakula kwani hawataki
kutumia kitu chochote cha wenyeji ili kuepuka hujuma kwenye mechi hiyo
itakayochezwa Jumapili usiku.
“Tumepata ushindi wa kihistoria lakini hatuwezi
kukaa chini kushangilia, kwa sasa tunatakiwa kuanza maandalizi ya mechi
ya marudiano ndio maana naondoka kuelekea Misri kufanya mambo,”
alisisitiza Seif.
“Tunatakiwa kujipanga vizuri kabla ya mchezo wa
marudiano, kabla ya timu kufika kuna mambo ambayo ni lazima tuyaweke
sawa ili kukamilisha lengo letu la kusonga mbele, kuna haja ya kuandaa
sehemu salama ya kufikia kikosi chetu, wapi tutafanyia mazoezi ni lazima
tuyafanye hayo yote sasa, hawa jamaa inabidi kuwa nao makini sana.”
Akizungumza na Mwanaspoti, Abdallah Bin Kleb
alisema: “Tunajua wenzetu watakuwa wamejiandaa kuhakikisha wanatufunga
nyumbani kwao, hivyo tumeanza maandalizi rasmi katika kuhakikisha
tunapata ushindi ugenini baada ya kuwafunga nyumbani.
“Kiongozi mmoja anatangulia Misri, timu inaondoka
Alhamisi na kufika Ijumaa, itachelewa kuondoka kutokana na mechi hiyo
kuchezwa Jumapili.”
Kocha Al Ahly aitisha
Kocha Mkuu wa Al Ahly, Mohamed Youssef, amesema kuwa hatakubali kufungwa mara mbili na Yanga, ugenini na nyumbani.
“Nimeziona mbinu za wapinzani wangu Yanga, sina
hofu ya mechi ya marudiano tutakayorudiana na wapinzani wetu, nimepanga
kwenda kukiboresha kikosi changu ili mechi ya marudiano tushinde,”
alisema.
RSS Feed
Twitter
7:01 AM
Unknown
Posted in
0 comments:
Post a Comment