ENGLAND
KOCHA Mkuu wa Manchester United, David Moyes, ametetea kiwango kikubwa cha mshahara wa supastaa, Wayne Rooney, katika klabu hiyo ya Old Trafford baada ya kusaini mkataba mpya.
Staa huyo Mwingereza, amesaini mkataba utakaomshuhudia akilipwa mshahara wa Pauni 300,000 kwa wiki. Lakini, baada ya watu kuanza kujadili mshahara wa mchezaji huyo, Moyes ameingilia kati kwa haraka na kutaka straika wake aachwe na mambo yake.
Alisema: “Hebu tazama pesa zinazoingizwa na klabu
kwenye mchezo huu kutokana na mapato ya televisheni. Tazama idadi ya
watu wanaopata ajira kwenye mchezo wa soka kwa sasa.
“Watu hao ni kama Rooney na wanalipwa mishahara
mikubwa. Kwa hilo ndiyo maana analipwa vizuri. Tazama pia pesa
zinazotengenezwa na klabu kama Manchester United ambayo inajaza uwanja
kila wiki, inapata mikataba mizuri ya kibiashara kila kona.
“Watu wanahitaji vitu kama hivi. Hii inaonyesha
kwamba kama mchezaji utakuja Manchester United na kufanya majukumu yako
vizuri, basi siku moja utafanywa kuwa mchezaji unayelipwa pesa nyingi
kuliko wengine wote.”
Rooney juzi Jumamosi alionyesha thamani ya pesa anazolipwa baada ya kufunga bao safi kwenye ushindi wa 2-0 dhidi ya Crystal Palace kwenye Ligi Kuu England.
Ushindi huo ulikuwa muhimu kwa timu yake na
umewawezesha kupanda hadi nafasi ya sita kwenye msimamo. Bao jingine la
wababe hao wa Old Trafford lilifungwa na straika, Robin van Persie.
0 comments:
Post a Comment