Kiburi cha Yanga chawakera Waarabu Cairo
Mshambuliaji wa Yanga, Emmanuel Okwi (kushoto) akiwapita walinzi wa Al Ahly ya Misri katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam juzi Jumamosi
YANGA imeonyesha kiburi baada ya kutibua na kuipiga chini dili ya kampuni moja ya Arabuni ambayo walikubaliana awali kuonyesha mechi zao dhidi ya Al Ahly kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga imekosa kiasi cha dola 70,000 ambazo ni
zaidi ya Sh 112 milioni baada ya kushindwa kuafikiana na Kampuni ya MGB
Misri kuhusu kuonyeshwa moja kwa moja michezo hiyo ya raundi ya kwanza
ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika makubaliano ya awali, Yanga ilipaswa kulipwa dola 35,000
kabla ya mechi na kiasi kingine kilipwe baada ya mechi hiyo iliyoisha
kwa Wanajangwani kuibuka na ushindi wa bao 1-0.
Akizungumza na Mwanaspoti, ofisa wa MGB, Francis
Gaitho, alisema kampuni hiyo iliingizia Yanga kiasi hicho cha fedha
kupitia akaunti yake ya Misri lakini ikataka ilipwe fedha zote kabla ya
mchezo huo.
Kutokana na mambo kwenda kinyume, MGB ilibidi
ifanye jitihada mbalimbali za kuilipa Yanga lakini mambo yalipoenda
kombo ikabidi wachukue dhamana kwa Ubalozi wa Misri nchini na Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF), hata hivyo Yanga ilikataa dhamana hizo.
Kwa kuwa timu ya kurekodi mchezo huo kutoka Misri
ingechelewa kutokana na ratiba za ndege, kampuni hiyo iliamua kutoa
tenda hiyo kwa Star TV waweze kurekodi na kuwarushia halafu wao
wasambaze kwa nchi za Afrika Kaskazini na Magharibi. Yanga haikukubali
Star TV kufunga vifaa vyao uwanjani hapo kwa muda uliopangwa na hata
iliporuhusu muda ulikuwa umeisha kuweza kufunga vifaa na kurusha mchezo
huo.
“Nasikia viongozi wa Yanga ni matajiri lakini
sielewi kwa nini dola 35,000 ziliwanyima usingizi, ni kiasi kidogo sana
cha fedha lakini hawakujua thamani ya mchezo ule na kuamua kukataa
kuonyesha mechi,” alisema Gaitho.
Alisema hiyo ilikuwa nafasi pekee kwa wachezaji wa
Tanzania kujiuza kimataifa kwani vipaji vyao vingeonekana kote duniani
na wangeweza kuitwa na klabu mbalimbali za ndani na nje ya Afrika.
“Yanga imewanyika haki watu wa Misri na Tanzania
kutazama mechi ile ya kihistoria, Yanga ingejitangaza kote duniani kwani
watu wangetaka kuona ni timu gani iliyowafunga mabingwa wa Afrika,
hivyo bao lake pekee lingetazamwa kila mara ulimwenguni,” alisema
Gaitho.
Mwanaspoti lilipowasiliana na Katibu Mkuu wa
Yanga, Beno Njovu alisema apigiwe baadaye pindi atakapopata taarifa
rasmi kuhusu sakata hilo. Hadi jana saa 10:52 jioni katibu huyo hakuwa
akipatikana katika simu na hata viongozi wengine hawakupatikana.
Baadaye saa 10:57 alipatikana Makamu Mwenyekiti wa
Kamati ya Mashindano, Moses Katabalo ambaye alisema: “Tafadhali mtafute
katibu kuhusu hilo suala, sipo katika nafasi ya kuzungumzia.”
Nyota wa zamani wa Al Ahly, Zakaria Nassef amelalamikia kitendo cha Yanga kuwabania kuona mechi hiyo aliyoiita ya karne.
0 comments:
Post a Comment