Thursday, February 13, 2014

            Simba, Yanga staili mpya

    

                        Kocha Hans akitoa maelekezo kwa mchezaji wake wa Yanga  

KATIKA kuhakikisha wachezaji wao wanashika mafunzo kikamilifu, makocha Wazungu, Zdravko Logarusic (Simba) na Hans Pluijm (Yanga), wamekuja na staili za kisasa zaidi ambazo ni ngeni kwa timu za soka za Tanzania.
Makocha hao wamekuwa wakifundisha kwa staili mbili, kwanza wanaanza kwa kusisitiza vitendo na baadaye wanatumia ubao wa kuandikia kuwaelekeza wachezaji kwa karibu zaidi ili kila mmoja aelewe kiundani.
Staili hiyo imekuwa ikitumiwa na makocha hao tangu waanze kazi kwenye timu hizo kongwe ambazo zinapashia kwenye viwanja vya kuazima.
Kwenye Uwanja wa Kinesi, Ubungo jijini Dar es Salaam, Logarusic amekuwa akitumia ubao kwa dakika kumi kuwafundisha wachezaji wake baada ya kusimamisha mchezo na kuwakusanya, wachezaji humzunguka.
Kwa upande mwingine, Pluijm amekuwa akitumia muda wa dakika 15 katika mazoezi yake kwa ajili ya kuzungumza na wachezaji kwa karibu zaidi na kutoa maelekezo kwa maandishi ubaoni.
Yanga iliyokuwa ikifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam inaondoka leo Alhamisi kwenda Comoro kurudiana na Komorozine katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Pluijm amekuwa akiwasimamisha wachezaji sehemu moja na huku akizungumza nao na wakati mwingine kumwelekeza mmoja mmoja pembeni akisaidiwa na Kocha Msaidizi, Boniface Mkwasa. Amekuwa akiwaelekeza makosa ambayo ameyaona ndani ya uwanja na namna ya kufanya ili wafanikiwe zaidi na wakimaliza, wanafanya mazoezi ya mwisho kwa vitendo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mkwasa alisema: “Tunafanya hivi kwa ajili ya kuelekezana upungufu na namna ya kuutatua, kama tutafanya tu mazoezi ya kucheza bila darasa hatuwezi kufanikiwa.”

 

0 comments:

Post a Comment

Designed by Adamu Mwanakatwe