Mzungu aipangua first eleven Simba
Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic
KOCHA wa Simba, Zdravko Logarusic, ametangaza mabadiliko makubwa katika kikosi chake kitakachoivaa Mbeya City Jumamosi wiki hii.
Amesema ataingiza sura tatu mpya na kubadili uchezaji huku akiwataka mashabiki kutoshituka kwani imebidi iwe hivyo.
Simba haikufanya vizuri katika mechi mbili za
ugenini baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar mjini
Morogoro kisha kulala bao 1-0 mbele ya Mgambo JKT mjini Tanga.
Kwa sasa Simba ipo nafasi ya nne katika msimamo wa
Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 31 wakati Mbeya City ni ya tatu ikiwa na
pointi 34, zote zimecheza mechi 17.
Katika kikosi chake, Logarusic, amewaweka kikosi
cha kwanza William Lucian ‘Gallas’, Said Ndemla na Henry Joseph huku
akiwaondoa kikosini Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Haruna Shamte na Awadh
Juma.
Hivyo kikosi cha sasa cha Simba kitaundwa na Ivo
Mapunda, Gallas, Henry, Joseph Owino, Donald Mosoti, Jonas Mkude,
Ramadhan Singano ‘Messi’, Ndemla, Amissi Tambwe, Amri Kiemba na Haruna
Chanongo.
Katika mazoezi ya timu hiyo yaliyoshuhudiwa na
Mwanaspoti, Logarusic, alionekana amepanga kikosi hicho huku akiwapa
maelekezo ya kila mara wale walioingia kikosini kwa mara ya kwanza.
Kikosi cha mwisho cha Simba kilichocheza dhidi ya
Mgambo kilikuwa; Mapunda, Shamte, Baba Ubaya, Owino, Mosoti, Mkude,
Kiemba, Awadh, Messi, Tambwe na Ali Badru.
“Ninachotaka ni ushindi, nitampa nafasi mchezaji
ambaye atawajibika ipasavyo uwanjani si zaidi ya hapo, kama umeona
mabadiliko hayo ni kweli nimeyafanya kwa manufaa ya timu yangu,” alisema
Logarusic ambaye ni raia wa Croatia.
Baba Ubaya sasa anapikwa ili acheze nafasi ya
winga wa kulia, wakati kiungo Henry Joseph ataanza kuchezeshwa beki wa
kushoto kuanzia wikiendi hii.
Logarusic alikuwa akimwelekeza Baba Ubaya mahali
pa kusimama kama winga pia jinsi ya kucheza kwa kusaidia sehemu ya
kiungo. Kocha huyo pia alikuwa akimpa maelekezo Henry Joseph
aliyechezeshwa beki wa kushoto nyuma ya Haroun Chanongo.
“Issa (Baba Ubaya) nimeona anafaa kucheza winga
kuliko beki, ndiyo maana umeona nampa mazoezi ya kucheza nafasi hiyo.
Hii ni hali ya kawaida katika timu hasa wakati kama huu tunaotafuta
matokeo kwa nguvu, Henry ni mzoefu nataka kutumia uzoefu wake kuipa
mafanikio Simba, ataweza kucheza beki hakuna tatizo.”
0 comments:
Post a Comment