Adamu Mwanakatwe
RAFIKI yangu mmoja, Abdul Nsembo kiutani ana tabia ya
kukuhesabia vitu alivyokuzidi maishani. Mwishowe kabisa anakwambia
amekuzidi hata dhambi zake. Kwamba anazo nyingi kuliko zako.
Ni kama Wamisri. Wana uwezo mkubwa wa kutuhesabia
jinsi walivyotuzidi kwa kila kitu. Uchumi, soka, mipango, historia. Na
hata dhambi nazo wametuzidi. Historia yao ya mauaji ya kinyama siku za
karibuni yanadhihirisha hilo.
Na hata wakati Al Ahly ya Misri ikijiandaa kucheza
na Yanga katika pambano lake la raundi ya kwanza la Ligi ya Mabingwa
Afrika, inaonekana kama vile wameizidi Yanga kila kitu. Kuanzia soka
lao, uchumi wa klabu na hata dhambi.
Al Alhy wapo hapa jijini Dar es Salaam. Wamejikita
katika kuichunguza Yanga. Hata hivyo asilimia 90 ya hali halisi ni
kwamba wanapewa nafasi kubwa ya kuitupa Yanga nje ya mashindano. Lakini
wameiheshimu Yanga.
Yanga hawajali sana. Wao wapo wapo tu. Furaha yao
kubwa katika siku za karibuni ilikuwa ni kuwachapa Mbeya City. Baada ya
hapo wakafurahia sare ya watani zao Simba na Mtibwa pale Uwanja wa
Jamhuri, Morogoro.
Baada ya hapo wakafurahia ushindi wa mabao 7-0
dhidi ya vibonde Komorozine katika pambano ambalo wachezaji watatu wa
Yanga wangeweza kucheza mechi wakiwa wamefumba macho na bado timu yao
ingeshinda.
Baada ya hapo Yanga wamejikita katika kufurahia
kichapo cha bao 1-0 ambacho watani zao wamepata kutoka kwa Mgambo.
Lakini wakati Yanga wakifurahia kichapo cha Simba kwa Mgambo, kocha
Msaidizi wa Al Ahly, Ahmed Ayoub na skauti mkuu wa timu hiyo walikuwa
Uwanja wa Chamazi kuomba kutumia huduma za kisasa za uwanja huo wakati
wa mechi yao dhidi ya Yanga.
Hapa ndipo unapogundua kuwa tunaishi katika dunia
mbili tofauti. Mechi ya Yanga na Comoro ni wazi kuwa imeshamalizika.
Lakini ni namna gani Yanga wanajiandaa kucheza na Al Alhy? Hauwezi
kujua.
Kabla hata Yanga hawajaingiza timu kucheza na
Comoro ilikuwa ni wazi kwamba Wacomoro walikuwa wamejifia. Walipaswa
kuanza kuichunguza Al Ahly mapema zaidi. Walipaswa kujua timu yao
itafikia hoteli gani Cairo, itafanyia mazoezi wapi, na hoteli yao iko
umbali gani kutoka uwanjani.
Walipaswa kujua ni timu gani wanaweza kucheza nayo Afrika Kaskazini kabla ya kwenda Cairo.
Sijui kama wamejipanga kwa hili mapema, lakini kwa
wenzetu mechi ya soka ina maandalizi ya muda mrefu. Kwa sisi Watanzania
utakachoweza kusikia baada ya Yanga kuitoa rasmi Comoro ni kwamba
‘Tunamtafutia kocha mikanda ya Al Ahly’.
Hapo unakuta kocha anatafutiwa mikanda ya Al Ahly
ya misimu mitatu nyuma. Unakuta baadhi ya wachezaji wamehama, kocha
amebadilika, timu imeingiza wachezaji chipukizi. Na bado unajisifu kuwa
umeisoma timu katika mkanda wa video.
0 comments:
Post a Comment