Mafuriko ya Yanga yaisomba Simba Dar
MAFURIKO ya ushindi wa kishindo wa Yanga wa mabao 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting
juzi Jumamosi, jana Jumapili yaliizoa Simba kwenye Uwanja wa Taifa
baada ya Mnyama kukubali kipigo cha mabao 3-2 mbele ya JKT Ruvu kwenye
uwanja huo huo.
Simba waliingia uwanjani wakiwa na malengo mawili.
Kwanza kujibu mapigo kwa Yanga kwa kuichapa kipigo cha maana JKT Ruvu
ili kujikita kwenye nafasi ya tatu, lakini pili, kuisulubu timu hiyo ya
jeshi ambayo katika mchezo uliopita ilipigwa mabao 6-0 na Prisons mjini
Mbeya.
Wachezaji waliuchukulia mchezo huo laini lakini
JKT walipoanza kushinda Simba wakapoteana na kumuacha Kocha mpya wa JKT
Ruvu, Fred Minziro akicheka na kuonyesha mbwembwe za kila aina kwenye
benchi lake.
Ukuta Simba
Ukuta wa Simba pamoja na makipa wao wameendelea
kuigharimu timu hiyo baada ya kuruhusu mabao sita katika mechi nne
mfululizo ambazo wameambulia pointi mbili huku Azam iliyokuwa kwenye
uwanja wake wa Azam Complex, ikikubali sare ya mabao 2-2 mbele ya
Prisons.
Matokeo ya jana yameibakisha Azam kwenye nafasi ya
pili katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 37 na Yanga pointi 38
kileleni na Simba itaendelea kushika nafasi ya nne ikiwa na pointi 32 na
Mbeya City nafasi ya tatu kwa pointi 35.
Katika mechi ya jana, ukuta wa Simba ulijengwa na mabeki Wiliam Lucian ‘Gallas’, Joseph Owino, Donald Mosoti na Henry Joseph ambaye alizidiwa kushoto na kusababisha JKT Ruvu kupata mabao yote kupitia upande wake.
Mabeki hao na makipa, Ivo Mapunda na Yaw Berko wameigharimu Simba tangu mechi yao ya Mtibwa Sugar ambayo walitoka sare ya bao 1-1, Mgambo Shooting walifungwa bao 1-0 na kutoka sare ya bao 1-1 na Mbeya City.
JKT walianza kuiandama Simba dakika ya sita
kupitia kwa Idd Mbaga aliyekosa bao la wazi akiwa na Berko akishindwa
kuunganisha pasi safi ya Amos Mgisa aliyemtoka Henry Joseph ambapo shuti
la Mbaga lilidakwa na Berko huku mwamuzi David Paul akimpa kadi ya njano Damas Makwaya.
Wanajeshi wachachamaa
Wanajeshi hao walianza kuinyanyasa Simba kwa
kuifunga bao la kwanza dakika 13 kupitia kwa Hussein Bunu aliyepokea
pasi safi ya Mbaga, ingawa timu zote zilikuwa zikishambaliana kijanja na
Amissi Tambwe akidhibitiwa na mabeki wa JKT.
Kocha wa Simba Zdravko Logarusic, aliamua kufanya
mabadiliko dakika 22 kwa kumtoa Said Ndemla ambaye nafasi yake
ilichukuliwa na Ally Badru. Dakika 29, Amri Kiemba alikosa mabao baada
ya kupaisha mipira aliyotengewa na Haroun Chanongo huku mwamuzi akitoa
kadi nyingine ya njano kwa Bunu wa JKT Ruvu ikiwa ni dakika ya 32 kwa
kosa la kupiga mpira nje bila kujali filimbi.
0 comments:
Post a Comment