INAWEZEKANA: Man City wanavyomhitaji kiungo wao Fernandinho
KWA sasa kiungo wa Manchester City, Fernandinho ni majeruhi.
Kiungo huyu amekuwa kati ya viungo bora katika Ligi Kuu England msimu
huu.
Ni mchezaji muhimu sana katika kikosi cha kwanza
cha Manchester City. Manchester City wameshindwa kutamba katika mechi
zao mbili za mwisho jambo ambalo limewashangaza mashabiki wengi wa soka
hasa wale wa timu hiyo.
Jumamosi iliyopita walitoka sare dhidi ya Norwich
na wote tunakumbuka, kwamba walifungwa na Chelsea katika uwanja wao wa
nyumbani wiki iliyopita!
Katika mechi hizi mbili, Fernandinho hajacheza kutokana na kuwa majeruhi na ni wazi kwamba pengo lake limedhihirika.
Naamini kocha wa Manchester City, Manuel
Pellegrini kushindwa kumpanga Fernandinho kutokana na kuwa majeruhi ni
moja ya sababu za Manchester City kupoteza pointi katika mechi za hivi
karibuni.
Katika misimu ya karibuni wachambuzi wengi wa soka
wanaamini kwamba Yaya Toure ni kiungo bora katika Ligi Kuu England. Ni
kutokana na uwezo wake mkubwa wa kushambulia na kukaba. Pia Yaya Toure
ana pumzi ya kutisha na huwa anakimbia kutoka 18 ya Manchester City
mpaka 18 ya timu pinzani. Hufanya hivyo mara nyingi na katika mechi
moja.
Waingereza wanawaita wachezaji kama Yaya Toure
“box to box players”- kwa maana ya mchezaji wa kutoka boksi hadi boksi.
Kuna wachezaji wachache kama Yaya Toure duniani, lakini, Fernandinho pia
ni “box to box player” na mchezo wake unafanana na ule wa Yaya Toure.
Fernandinho pia ana nguvu ya kutisha na tumeona
msimu huu kwamba Yaya Toure na Fernandinho wakicheza pamoja kuna timu
chache sana ambazo zinaweza kuwafunga Manchester City!
Kwa muda mrefu nimeamini kwamba Manchester City
wana kikosi bora katika Ligi Kuu England. Ni kwa kuwa timu hiyo ina
zaidi ya mchezaji mmoja mzuri katika kila nafasi.
Kwa mfano, hata kama Sergio Aguero ni majeruhi kwa
sasa, kuna washambuliaji wengi wenye uwezo wa kufunga magoli kama Edin
Dzeko, Negredo na Jovetic.
Lakini, katika nafasi ya kiungo wa kati tumeona
kwamba hakuna wachezaji wazuri sana nyuma ya Yaya Toure na Fernandinho,
huo ndio ukweli ambao unaonekana kudhihirika hususan katika kipindi
hiki. Ndio, Demichelis ameshawahi kucheza katika nafasi ya kiungo wa
kati wakati akiichezea Bayern Munich,
Lakini, katika misimu ya karibuni, Muargentina
huyu ameweza kucheza nafasi ya beki. Katika mechi dhidi ya Chelsea,
Demichelis alicheza katika nafasi ya kiungo wa kati.
0 comments:
Post a Comment