
UKISIKIA la kuvunda halina ubani ndio huku. Ni baada ya straika wa zamani wa Yanga, Jerry Tegete, kulipiga teke fuko la fedha.
Ipo hivi; Kocha wa Coastal Union, Jackson Mayanja,
alidhamiria kumsajili Tegete kutokana na kuvutiwa na kipaji chake na
alikuwa tayari kufanya lolote ili straika huyo aichezee timu yake.
Lakini baada ya Tegete kumdengulia, ameamua kuachana naye. Tegete ametangaza kustaafu kucheza kwa mwaka mmoja.
“Tegete (Jerry) amenishangaza sana. Sijui tatizo
ni nidhamu, kukata tamaa au kutojitambua. Sijaelewa kwanini hataki
kucheza mpira wakati umri wake bado ni mdogo na ana kipaji kizuri,”
Mayanja alisema.
“Mchezaji hawezi kustaafu kwa mwaka mmoja halafu
akarejea uwanjani na kucheza katika kiwango kile kile. Mpira hauhitaji
mapumziko ya aina hiyo. Kwanza mchezaji anapopumzika anaweza kuongezeka
uzito haraka, lakini pia anakuwa na hatari ya kuendekeza mambo ya dunia.
“Sijui ni kivipi Tegete ataweza kurudi kiwanjani
na awe vizuri. Nilimpa fursa na haitaki ingawa nilikuwa naamini ni
mchezaji mzuri na angeweza kubadilika.”
Tegete ameliambia wazi Mwanaspoti kuwa hana mpango
wa kucheza soka la ushindani kwa sasa na kwamba amepanga kuendelea na
shughuli nyingine huku akidai kuwa amekataa ofa nyingi alizokuwa amepata
kwa sababu hana mipango ya kucheza kwa sasa.
Tegete amekua akihusishwa na kujiunga na Mwadui
lakini Coastal Union ilikuwa tayari kwa gharama yoyote kumnasa straika
huyo wa zamani wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’.
0 comments:
Post a Comment