
HATIMAYE Azam imeweka historia kwa kulibeba kwa mara ya kwanza taji la michuano ya Kombe la Kagame iliyomalizika juzi Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Awali mashabiki walishuhudia ushindani ambao
ulilifanya taji la michuano hiyo kuwa gumu kubashiri kwamba nani
angeweza kuibuka mshindi hasa kwa timu za Gor Mahia ya Kenya, KCCA ya
Uganda, Al-Khartoum ya Sudan na wenyeji Azam.
Hali hiyo ilitokana na namna ushindani ulivyokuwa
na wengi walipata tabu kuitabiria Azam ubingwa hata baada ya ushindi
wake dhidi ya Yanga katika mechi ya robo fainali.
Kwa baadhi ya mashabiki ushindani ambao ulianza
kuonekana katika hatua ya robo fainali ni kati ya mambo ambayo
yanapendeza kuonekana katika mashindano ya Kombe la Kagame tangu hatua
ya makundi.
Hatua ya makundi isiwe mteremeko kwa baadhi ya
timu kujihakikishia ushindi wa mabao mengi kwani jambo hilo linachangia
kushusha au kupoteza hadhi ya mashindano haya ambayo yanashirikisha timu
za nchi tofauti.
Ni matumaini yetu kwamba katika mashindano yajayo
timu zitajipanga kuhakikisha zinatoa ushindani jambo ambalo litayafanya
mashindano kuwa na mvuto na kuanzia hatua za mwanzo na hivyo kusaidia
kuinua soka la Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Kwa Azam ushindi
ambao wameupata ni kati ya mambo ambayo mashabiki wa timu hiyo na
mashabiki wa soka nchini kwa jumla wamekuwa wakiyasubiri au kuyatarajia
kwa muda mrefu sasa.Azam ni timu ambayo imefanya uwekezaji wa hali ya
juu kuanzia kwa wachezaji na mambo mengine ya msingi katika soka hivyo
ubingwa wa Kagame ni haki yao na ni kati ya mambo ambayo yanapendeza
kusikia wameyafanikisha.
Hata hivyo, pamoja na ukweli huo, pia tungependa
kuwakumbusha viongozi na wachezaji wa Azam kwamba bado wana kazi ya
kufanya baada ya Kombe la Kagame.
Kwa hadhi na uwekezaji uliofanywa na Azam ni
muhimu wakaweka mikakati ya kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye
mashindano ya Afrika.
Kombe la Shirikisho au Ligi ya Mabingwa Afrika ni
aina ya mashindano ya kiwango cha Azam kushiriki na kuhakikisha
wanafanya vizuri na si kubweteka na Kombe la Kagame. Ni kweli kwamba
Kombe la Kagame ni faraja mojawapo kwa timu hiyo na mashabiki wake
lakini ni vyema timu hiyo ikaanza kusaka heshima yake Afrika, hiyo ndiyo
hadhi yao na si Kagame au Ligi Kuu Bara pekee. Azam hii inatakiwa
kuanza kujifananisha na timu za Esperance au Etoile du Sahel za Tunisia
au TP Mazembe ya Kongo na timu nyingine kubwa Afrika.
0 comments:
Post a Comment